2012-12-31 07:54:11

Vijana mkimbilieni Yesu Kristo mnapokuwa katika giza, upofu wa imani na magumu ya maisha!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, tarehe 29 Desemba 2012, alijiunga na umati mkubwa wa vijana zaidi ya arobaini elfu wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Ulaya, waliokuwa wanashiriki katika mkutano wa thelathini na tano wa sala kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican, kielelezo cha imani ya mitume waliyoyamimina maisha yao kwa ajili ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Anawapongeza vijana hawa kwa kutaka kumwilisha imani kwa Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao kama sehemu ya mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Baba Mtakatifu anasema, hii ni mara ya nne kwa Jumuiya Taizè kukutana mjini Roma na kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro yuko pamoja nao katika hija ya imani hapa duniani kwani hata yeye anachangamotishwa kuwa ni hujaji wa imani katika Kristo, kama alivyowahi kusema Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili. Jumuiya ya Taizè ilianzishwa yapata miaka sabini iliyopita na Fra Roger na tangu wakati huo, imeendelea kukusanya vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaotafuta maana ya maisha, katika sala sanjari na kujenga uhusiano binafsi na Mwenyezi Mungu.

Huu ukawa ni mwanzo wa Jumuiya ya Taizè, kielelezo makini cha ushuhuda wa amani, upatanisho unaopata chimbuko lake katika majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika utakatifu wa maisha; daima wakitafuta kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo.

Majadiliano ya kiekumene hayana budi kumwilishwa katika undani wa mwamini kwa njia ya ushuhuda na umati huu wa vijana anasema Baba Mtakatifu ni mashahidi wa ujumbe wa umoja wa Kanisa; dhamana inayopewa kipaumbele cha pekee na Kanisa Katoliki kwa njia ya upatanisho ili kupata umoja mkamilifu miongoni mwa wafuasi wa Kristo: yaani waamini wa Makanisa ya Kiprotestanti na Kiorthodox.

Yesu alipowauliza wanafunzi wake kwake kwamba, watu wanasema kuwa Yeye ni nani, Petro alimjibu kwa uhakika kwamba, Yeye ni Kristo Mwana wa Mungu aliyehai; jibu ambalo lilifumbata hija ya maisha yake yote hapa duniani, changamoto hata kwa vijana kutoa jibu makini kuhusu imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kwa ujasiri mkubwa bila ya woga, ili kupata maana halisi ya maisha ya ujana wao. Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, iwachangamotishe kumpenda Mungu na jirani.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawaalika vijana wa Taizè wakati wa sala na tafakari zao kutoa nafasi ya pekee kwa Kristo, Mwanga unaoangazia mapito ya maisha yao na kamwe wasitawaliwe na magumu pamoja na masumbuko yanayowapata watu wasiokuwa na hatia; daima wamkimbilie Yesu wanapojikuta katika giza na upofu wa imani, kwani Mungu daima yuko pamoja nao!

Anawakirimia furaha, faraja na umoja ndani ya Kanisa. Anazishukuru Familia na Jumuiya mbali mbali za Kikristo mjini Roma zilizoonesha kwa namna ya pekee, ukarimu na mshikamano kwa vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè, kwani kwa pamoja wanajenga Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Ni wajibu wa kila kijana kutumia karama na vipaji vyake kwa ajili ya ujenzi wa umoja wa Kanisa, wakiwa tayari kutangaza Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia. Ukimya na nyimbo za vijana wa Taizè zimepamba Makanisa makuu ya Roma yakionesha matumaini na sifa kwa Mwenyezi Mungu ambaye kamwe hawezi kuwatupa!

Anawawachangamotisha vijana kuwa ni mwanga kwa wale wanaowazunguka, daima wakitafuta mafao ya wengi, na kushiriki katika mchakato wa kudumisha misingi ya amani na mshikamano kati ya binadamu, wakiwaelekeza jirani zao ile njia inayokwenda kwa Mungu.








All the contents on this site are copyrighted ©.