2012-12-31 15:43:43

Sala ya mwadilifu mdhulumiwa!


Zaburi hii ni kilio cha anayeonewa. Muhusika ni yeye mwenyewe au mwakilishi wa wengine. Maisha yake yapo katika hatari kutokana na watu wanaomzunguka na ambao mwanzoni walikuwa rafiki zake. Leo hii wimbo huu waweza kuimbwa na yeyote kati yetu anayetambua kwamba anaonewa.

Anaanza kwa kumwita Mungu ajitokeze kama shujaa: Uishike ngao na kigao. Inaonekana mtunzi na wenzake wamegeuka wakimbizi milimani, kutokana na kuwahofia watesi wao. Maadui hawa wapo kila mahali: mahakamani ni washitaki wao, maadui zao vitani, ni wawindaji wanaotupa nyavu na kuchimba mashimo kuwatega, ni majambazi mitaani, ni wanyama wakali mwituni. Watesi hawa wanavumisha matusi na maneno ya kejeli kwao, kote kote hatari inawazunguka. Shaka yake anaieleza kwa hemo la kukata tamaa: Bwana, hata lini utatazama?

Mtunzi wetu picha anayotuchorea ni kuwa ni mtu mwadilifu na mpole anayefuata nyendo za baba zake. Anachoomba ni kuwa yeye na wenzake waachwe huru. Kwa kutumia kanuni ya jino kwa jino, anawaombea watesi wao wapate fadhila kama wanayowapatia wao.

Tunafundishwa naye jinsi ya kuwafariji watu wenye huzuni, kwani hata yeye ameonja huzuni. Tunapaswa kuhuzunika na wenye kuhuzunika, huzuni ya kweli na si ya mamba. Mtu mmoja alikuwa na uchungu mkubwa na kuuliwa kinyama kwa mtoto wake mpenzi. Wakati wa ibada ya maziko, mwongoza ibada alipotoa chozi kutokana na ukatili huo, mzazi wa mtoto huyo, moyo wake ukafunguka kwa tulizo la amani. Tukumbuke “Heri walio na huzuni, maana hao watatulizwa” (Mt 5:4).

Mtunzi anaahidi kama ataokolewa toka katika midomo ya simba, ataenda mbele ya kusanyiko kumtolea Bwana sifa ya shukrani. Tunakumbushwa kuwa nasi tu viungo katika mwili wa Kristo, na tunapopata fadhila fulani tusikose kuwashirikisha wengine furaha yetu.

Maneno Ewe! Ewe! Jicho letu limeona! Ni msemo wenye kuonesha dharau toka kwa wajinga ambao wamemwinukia mteswa wetu. Leo hii tunaweza kuyaweka katika msemo mmoja, mteswa wetu anaambiwa ‘amefulia.’ Mbaya zaidi, alisingiziwa mengi na mashahidi wa uongo walijitokeza dhidi yake. Hali hii ndiyo iliyompata Yesu wa Nazarethi (soma Mt 26:57-62).

Kwa jitihada kubwa anamsihi Bwana ‘umeona,’ ‘usiwe mbali,’ ‘amka’ ili amsaidie. Tunakumbushwa naye jukumu letu la kukumbuka kuwa watu wa shukrani kwa wale waliokuwa nasi tulipokuwa katika shida, iwe ya binafsi au ya taifa. Kwa namna ya pekee anahitimisha kwa kubainisha kwamba wakishinda shida yao, hawatajisifu wenyewe, bali waukumbuka mkono mwema wa Mungu kwa shukrani!








All the contents on this site are copyrighted ©.