Utukufu kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema ni ujumbe unaoendelea
kusikika masikioni mwa mwengi wakati huu wa maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli, lakini
kwa bahati mbaya dunia bado inaendelea kushuhudia vita, migogoro na kinzani za kijamii.
Fumbo la Umwilisho linapata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo
na ufufuko wa Kristo.
Mwenyezi Mungu ameweza kuupatanisha ulimwengu pamoja
naye; changamoto kwa binadamu kuendelea kujipatanisha wao kwa wao, ili dunia iweze
kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kwani bado chuki na uhasama vinaendelea kutawala
katika mioyo ya watu na kwamba, amani ya kweli inaonekana kuwa mbali kutokana na misimamo
mikali ya kiimani pamoja na uchu wa mali na madaraka.
Imekwishagota miaka 1700,
tangu Mfalme Costantino mkuu alipotoa ruhusa ya uhuru wa kidini kwa watu wote kwa
Tamko la Milano, kunako mwaka 313 Baada ya Kristo, bado kumekuwepo kwa madhulumu ya
kidini na waathirika wengi ni waamini wa dini ya Kikristo kama takwimu zinavyonesha
kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Hii ni sehemu ya ujumbe wa Kipindi cha
Noeli uliotolewa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwa Kanisa Kiorthodox la Costantinopoli
kwa waamini wa Kanisa lake pamoja na watu wote wenye mapenzi mema. Anasema, athari
za myumbo wa uchumi kimataifa ni matokeo ya ubinafsi, uchoyo pamoja na kukumbatia
uchumi wa kibepari unaongalia mtaji na faida kubwa hata kwa gharama ya maisha ya watu
wengi.
Hizi ni dalili za kumong’onyoka kwa maadili na utu wema na watu wanadhani
kwamba, soko huria lisilozingatia maadili, sheria na kanuni za fedha ni mkombozi wa
uchumi na soko la dunia. Lakini hii ni ndoto inayoendelea kuwatumbukiza watu wengi
katika umaskini wa kipato na ki hali sanjari na vitendo vya jinai vinavyovuka mipaka
ya kitaifa na kimataifa. Matukio yote haya ni hatari kwa amani na usalama wa Jumuiya
ya Kimataifa.
Kanisa la Kiorthodox linaendelea kufuatilia matukio mbali mbali
ya vita, kinzani za kijamii, kisiasa na kimaadili pamoja na maafa asilia mambo ambayo
yanatoa changamoto kubwa kwa waamini kujikita katika mshikamano wa upendo, kwa kuwafariji
na kuwasaidia jirani wanaoteseka kutokana na hali ngumu ya maisha.
Ndiyo maana
Kanisa la Kiorthodox linautangaza Mwaka 2013 kuwa ni Mwaka wa Mshikamano Kimataifa.
Lengo ni kushikamana katika mapambano dhidi ya umaskini na baa la njaa linaloendelea
kutesa mamillioni ya watu duniani sanjari na kusimama kidete kulinda na kutetea misingi
ya: haki, amani, usawa.
Patriaki Bartolomeo wa kwanza anahitimisha ujumbe wake
wa Noeli kwa kusema kuwa, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kuzaliwa na Bikira Maria
kwa njia ya Roho Mtakatifu ndiye Mkombozi wa dunia na Mfalme wa Amani, asaidie juhudi
za mshikamano wa kimataifa, uhuru, upatanisho, amani na matashi mema miongoni mwa
watu. Awe ni chemchemi ya uvumilivu, matumaini na nguvu thabiti.