2012-12-31 11:40:54

Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Sinodi za Maaskofu wa Afrika na Katekisimu Mpya ya ni sehemu ya hija ya imani katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani


Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki ni muhtasari makini wa Imani na mafundisho tanzu ya maisha ya Kikristo ambayo ni utekelezaji wa changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, takribani miaka 50 iliyopita. RealAudioMP3

Ni sehemu ya hija ya imani inayowachangamotisha waamini kusoma alama za nyakati, wakiwa tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu kadiri ya maisha na vipaumbele vyao.

Ni maneno ya Mheshimiwa Padre Dietrich Pendawazima, Makamu mkuu wa Shirika la Waconsolata, katika mahojiano maalum na Radio Vatican kuhusu viashilia vya imani kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Imani, unaowachangamotisha waamini kuhakikisha kwamba, wanaifahamu vyema imani yao, ili waweze kukua, kukomaa na kuimarisha, kiasi hata cha kutoka kifua mbele kuishuhudia kwa njia matendo adilifu.

Hija ya imani anasema Padre Pendawazima, inajionesha pia katika maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kuhusu Bara la Afrika yaliyokazia kwa namna ya pekee umuhimu wa Kanisa Barani Afrika katika mchakato wa uenezaji wa Injili hadi miisho ya dunia. Maadhimisho ya Sinodi ilikuwa ni alama ya mshikamano wa kiimani miongoni mwa Familia ya Mungu inayowajibika Barani Afrika.

Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika baada ya miaka kumi na tano tangu ilipoadhimishwa ile Sinodi ya kwanza iliyoletwa mwamko na ari mpya ya maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika, kwa wakati huu, waamini wanahamasishwa kuwa ni vyombo vya upatanisho, haki, amani na msamaha. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kuna dalili nyingi zinazoonesha hali tete ya imani, amani, matumaini na mapendo miongoni mwa Familia ya Mungu Barani Afrika. Changamoto zote hizi zinapaswa kufanyiwa kazi kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.







All the contents on this site are copyrighted ©.