2012-12-31 08:47:03

Jukumu la Familia kama Kanisa Dogo la Nyumbani katika Uinjilishaji Mpya!


Ndugu msilizaji wa Radio Vatican tunayo furaha kubwa leo kutafakari kwa pamoja Maadhimisho ya Siku kuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu katika mwaka huu wa imani. Mwaka unaotawaliwa na wazo la uenjilishaji mpya. Wazo la uenjilishaji mpya ni utume wa kanisa ambao unapata chimbuko lake kwa Kristo mwenyewe (Matayo 28: 19-20). RealAudioMP3
Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili alipolitaja wazo la Uinjilishaji mpya mwaka 1983 alikiri kuwa ni wazo lililopevuka katika maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unaotimiza miaka 50 ya uwepo wake na kupata msukumo mkubwa katika hati ya kichungaji ya papa Paulo VI Evangelii Nuntiandi yaani Uinjilishaji katika Ulimwengu mamboleo wa mwaka 1975.
Ni Uinjilishaji uleule Kristo alioufanya na alioamuru kanisa lake kuufanya kwa nyakati zote lakini unakuwa uenjilishaji mpya kwani ufanyike kwenye mazingira ya wakati wetu wenye makandokando yake na namna yake ya kufikiri na kutenda.
Kama ni utume wa kanisa basi basi ni utume wa Familia iliyo Kanisa dogo la nyumbani ambalo mfano wake ni wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu tunayoishangilia kwa namna ya pekee leo. Familia hii haikurudi nyuma kati ujenzi wa jumuiya ya kibinadamu, katika uzazi na malezi na ndilo Fumbo la Mungu kuwa mtu tunaloadhimisha wakati wa Siku kuu ya Noeli, Katika mahusiano na jamii pamoja na Mungu mwenyewe.
Kumbe mifano tuyoipata hapo inatuhakikishia kuwa Familia ni chimbuko la uenjilishaji mpya kwani Familia iliyo Kanisa dogo la nyumbani ndiye Muinjilishaji namba moja ndiyo maana hata Mtoto Yesu alipata nafasi ya kushikishwa katika mambo yote ya kiibada waliyofwata wazazi wake na akaongezeka katika kimo na hekima (Lk 2: 52). Pia Familia ni kilele cha Uinjilishaji kwani wakati wote familia takatifu ilijifunza kupokea na kutekeleza maagizo ya Mwenyezi Mungu.
Ndugu msilizaji, katika tafakari yetu ya mwaka huu wa imani ni vizuri tujipime kuwa ni kwa kiasi gani Familia yetu imebaki kuwa jumuiya inayoamini na enjilisha ndani na nje ya familia yetu? Ni kwa kiasi gani Familia yetu imeendelea kuwa chombo cha Sala na Liturujia ya Kanisa? Ni kiasi gani Familia yetu imeendelea kuwa chombo cha huduma kwa Mungu na kwa mwanadamu mwingine?
Hatujachelewa kufanya mabadilko ndio maana tumepata nafasi ya kuadhimisha sherehe hii ya familia takatifu katika mwaka huu wa imani na uenjilishaji mpya ili tujipange tena. Tukiwa na nia njema kwa maombezi ya familia takatifu tutafika.
Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi padre Raphael Mwanga, wa Jimbo Katoliki la Same, Taasisi ya Ndoa na Familia, Chuo Kikuu cha Kipapa Laterano- Roma.








All the contents on this site are copyrighted ©.