Familia inajukumu la kurithisha imani, kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani,
upendo na mshikamano wa kweli!
Askofu mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania katika mahojiano na Radio
Vatican anabainisha kwamba, Familia kimsingi inapaswa kuwa ni shule ya utakatifu,
haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati.
Hapa ni mahali
ambapo watu wanajifunza tunu bora za maisha ya kijamii, kiutu na kimaadili. Huu ndio
wajibu msingi wa wazazi na walezi katika familia, kiasi cha kuwafanya kuwa ni wajenzi
wa tunu hizi katika jamii inayowazunguka.
Lakini kwa bahati mbaya, mambo sivyo
yanavyokwenda katika hali halisi ya familia nyingi sehemu mbali mbali za dunia. Hii
inatokana na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa utandawazi, maendeleo ya
sayansi na teknolojia bila kusahau tabia ya ukanimungu inayopelekea watu wengi kumezwa
na malimwengu kiasi hata cha kusahau wajibu na dhamana ya familia ndani ya Kanisa
na Jamii kwa ujumla.
Askofu mkuu Lebulu anasema kwamba, kuna baadhi ya familia
zimeshindwa kurithisha tunu bora za maisha ya kijamii, kiutu na kimaadili na matokeo
yake dunia inakuwa ni uwanja wa fujo na vurugu. Baadhi ya wazazi wamechangia kuporomoka
kwa tunu msingi za maisha ya kifamilia na hivyo familia inakosa ile dhamana ya kuwa
ni shule ya utakatifu, haki na amani kama ambavyo ingetarajiwa kuwa!
Baadhi
ya wazazi wanawafundisha watoto wao kudharau na kubeza dini na imani za watu wengine
ndani ya Jamii, jambo ambalo ni hatari kubwa kwani ndiyo chanzo cha kinzani na migogoro
ya kidini inayoendelea kufuka moto sehemu mbali mbali za Bara la Afrika na duniani
kwa ujumla. Familia zisipotekeleza wajibu wake barabara, kuna hatari kubwa kwamba,
misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli itakuwa daima hatarini. Familia
zijengewe uwezo wa kurithisha tunu bora za maisha ya kijamii, kiutu na kimaadili,
ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.
Askofu mkuu Josephat
Lebulu anasema kwamba, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu iwe ni mfano na kielelezo
makini cha utekelezaji wa dhamana na majukumu ya kifamilia kwa kujikita katika kufanya
kazi kwa juhudi, bidii na maarifa; sala, kusoma na kulitafakari Neno la Mungu, kujitajirisha
kwa neema na Baraka za Mwenyezi Mungu kwa njia ya maisha ya Kisakramenti pamoja na
kumwilisha Imani katika matendo.
Jukumu kubwa la Familia za Kikristo wakati
huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Imani ni kuhakikisha kwamba, Familia zinakuwa
ni chemchemi za kurithisha imani tendaji kwa watoto wao.