2012-12-31 12:05:08

Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Siku ya Kuombea Amani Duniani 2013


Mama Kanisa anafunga mwaka 2012 kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema na ukarimu wake wote kwa kumwimbia utenzi wa shukrani, Te Deum, katika Ibada ya Masifu ya Jioni, itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican. Waamini watapata fursa ya kumwabudu, kumtukuza, kumwomba na kumshukuru Mungu kwa njia ya Yesu Kristo aliyeamua kubaki miongoni mwa wafuasi wake katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu.

Ni nafasi ya kuomba msamaha na huruma kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika Mwaka 2012 na hivyo kuomba tena huruma, neema na upendo wake, ili uweze kuwaongoza katika Mwaka Mpya wa 2013.

Tarehe Mosi, Januari 2013, Kanisa litaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu, "Theotokos" sanjari na Siku ya Arobaini na Tisa ya Kuombea Amani Duniani, inayoongozwa na kauli mbiu "Heri wapatanishi". Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu katika maadhimisho haya, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, itakuwa nawe bega kwa bega ili kuweza kukujuvya yale yanayojiri kutoka hapa mjini Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.