2012-12-29 07:32:52

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa ajili ya Siku ya 49 Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2013


Heri wapatanishi ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya 49 ya Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2013, sanjari na kumbu kumbu ya miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ulioimarisha utume wa Kanisa ulimwenguni, kwa kutambua kwamba, Familia ya Mungu inafanya hija ya kihistoria na binadamu wote kwa kushirikishana furaha, matumaini, machungu na magumu wakati ikiendelea kutangaza Habari Njema ya Wokovu na kutetea amani kwa wote. RealAudioMP3

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika ujumbe wake wa Siku ya Kuombea Amani Duniani inayokwenda sanjari na Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu, anabainisha kwamba, kuna kinzani na migogoro mingi inayoendelea kufuka moshi kutokana na kuongezeka kwa pengo kati ya maskini na matajiri, binafsi pamoja na athari za mfumo wa ubepari unaokumbatia mno faida.

Bado kuna vitendo vya kigaidi, makosa ya jinai, misimamo mikali ya imani inaendelea kuhatarisha amani na asili ya dini ya kweli inayopaswa kimsingi kukuza na kudumisha udugu na upatanisho kati ya watu. Mwanadamu ana wito unaobubujika kutoka katika undani wake unaotamani furaha na mafanikio.Mwanadamu anatamani kupata amani inayoambatana na haki na wajibu na kwamba, amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kauli mbiu ya Mwaka 2013 inapata chimbuko lake katika Heri za Mlimani: Heri wapatanishi maana wataitwa wana wa Mungu.

Hizi ni heri ambazo watabarikiwa kuzipata wale wanaojitoa bila ya kujibakiza katika kutafuta ukweli, haki na upendo, daima wakitambua kwamba, katika mahangaiko yote Mungu yuko pamoja nao na kuwa wakimkubali Yesu, Mungu kweli na Mtu kweli, wataweza kushiriki maisha ya kimungu, yaani neema yake, kwani Kristo ndiye anayemkirimia mwanadamu amani ya kweli, akikumbuka kwamba, amani ni zawadi inayoimarishwa kwa juhudi za kibinadamu, katika mchakato wa kuishi na kushirikishana na wengine, kama sehemu ya kanuni maadili ambazo kimsingi ni sheria ya Mungu iliyoandikwa katika moyo wa mwanadamu. Amani inajengwa na kudumishwa kwa kuzingatia akili na maadili.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na matunda ya kazi ya binadamu inayojionesha kwa kuwa na utilivu wa ndani, kwa kuishi vyema na jirani pamoja na kujali mazingira. Papa Yohane wa Ishirini na tatu katika Waraka wake Amani Duniani, Pacem In Terris anakazia mambo makuu manne ili kuweza kudumisha msingi wa amani: Ukweli, Uhuru, Upendo na Haki.

Hizi ni tunu msingi zinazomwezesha mwanadamu kuufahamu ukweli, uzuri na uwepo wa Mungu ambaye ni Muumbaji, kama njia ya kuendelea kuwa ni wapatanishi pamoja na kukuza majadiliano na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo. Amani inapatikana pale tu watu wanapotambua kwamba, wao mbele ya Mungu wanaunda Familia Moja ya binadamu inayoonesha uhusiano, wajibu na majukumu yak ila mtu. Amani inamwilishwa katika upendo kwa kushirikiana na kufanya kazi na wengine kwa ajili ya mafao ya wengi. Amani ni jambo linalowezekana na wala si wazo la kufikirika tu! Ndiyo maana Kanisa linaendelea kumtangaza Yesu Kristo msingi wa maendeleo endelevu na amani ya kweli. Ujenzi wa amani ni dhamana yak ila mtu!

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, wapatanishi ni watu wanaopenda fadhila ya upendo na kuendeleza maisha katika utimilifu wake, kwa kumheshimu mtu katika hatua zake mbali mbali za ukuaji na kamwe hawezi kukumbatia utamaduni wa kifo unaojidhihirisha katika sera za utoaji mimba. Ni mtu anayejali maendeleo pamoja na utunzaji wa mazingira. Ni vyema kuzingatia na kuheshimu kanuni na misingi bora ya maisha ya ndoa, kwa kutambua na kuthamini utume wake kwa Jamii husika mintarafu asili ya binadamu. Kanisa linaposimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa linafanya hivi kwa ajili ya mafao ya wengi, kinyume chake ni kupotosha ukweli, haki na amani. Watu wajenge dhamiri nyofu ili kusimama kidete kutetea zawadi ya maisha, ut una heshima ya binadamu dhidi ya vitendo vya utoaji mimba na kifo laini.

Uhuru wa kuabudu ni sehemu ya haki msingi za binadamu na kigezo muhimu katika kudumisha misingi ya amani kimataifa. Kuna dalili nyingi za uvunjifu wa misingi ya uhuru wa kuabudu, unaowazuia watu kutolea ushuhuda wa imani yao, kwa kuiungama na kuimwilisha hadharani na katika shughuli mbali mbali zinazopania kumletea mwanadamu maendeleo ya kweli. Sehemu mbali mbali za dunia, Wakristo wanaendelea kudhulumiwa.

Wapatanishi hawana budi kutambua kwamba, shinikizo linalotolewa katika maoni, sera na uhuru usiokuwa na mipaka lazima yajikite katika uwajibikaji, mshikamano, haki na wajibu. Kazi ni wajibu wa kijamii unaopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa kwa kupewa ujira unaostahili badala ya mfumo wa sasa kazi kuongozwa na mfumo wa uchumi huria na hivyo kupimwa kwa vigezo vya fedha na uchumi.

Kuna haja ya kuendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi wanapata fursa ya kazi kwa kuzinatia misingi ya maadili na tunu bora za maisha ya kiroho, kwa kutambua kuwa kazi ni kwa ajili ya mafao ya mtu binafsi, familia na Jamii katika ujumla wake. Kutokana na mwelekeo huu kuna haja ya kuwa na sera makini za fursa za ajira.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anahamasisha ujenzi wa amani ya kweli kwa njia ya miundo bora ya maendeleo na uchumi inayojikita katika mshikamano na mafao ya wengi kwa kutambua pia uwepo wa Mungu ili kupata maisha bora zaidi. Ili kuondokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, kuna haja kuwa na ugunduzi utakaobainisha mifumo mipya ya uchumi dhidi ya watu kutafuta faida kubwa inayogubikwa na ubinafsi na ulaji wa kupindukia. Watu wajitoe sadaka kwa kutumia vyema karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yao, ili yatumike kwa ajili ya mafao ya wengi, huku wakizingatia udugu; usawa na hali ya kutegemeana, daima wakilenga mafao ya wengi, kwa sasa na kwa kizazi kijacho.

Maendeleo ya uchumi, uzalishaji viwandani na katika sekta ya kilimo, yanahitaji kwa namna ya pekee kabisa uwepo wa misingi ya kimaadili kuhusu biashara na soko la fedha; uhakika na usalama wa chakula na mfumuko wa bei ya chakula; hali ambayo ni tete zaidi kuliko hata athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Wapatanishi wajenge na kudumisha mshikamano katika ngazi mbali mbali, hasa kwa kuwasaidia wakulima wadogo wadogo vijijini kutekeleza wajibu wao katika mazingira bora zaidi, wakilinda na kutunza mazingira sanjari na maboresho ya uchumi.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika ujumbe wake kwa Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2013 anagusia umuhimu wa elimu kama sehemu ya ujenzi wa utamaduni wa amani kwa kuiangalia familia pamoja na taasisi mbali mbali zinazopaswa kujikita katika kutafuta mafao ya familia na haki jamii bila kusahau umuhimu wa kuwa na elimu jamii makini. Familia ipewe kipaumbele cha kwanza katika majiundo ya mtu kwenye medani mbali mbali za maisha na kwamba, familia inawajibu wa kulinda na kutetea maisha, kulea, kutunza na kushirikishana.

Hapa ni mahali pa kujenga na kukuza utamaduni wa amani; kwa kutambua kuwa wazazi wanawajibu na dhamana ya kutoa elimu kwa watoto wao kimaadili na kiroho. Watoto warithishwe utamaduni wa kupenda na kuthamini zawadi ya maisha. Jumuiya za kidini zitekeleze pia wajibu wake kama sehemu ya mchakato wa Unjilishaji Mpya; daima wakijitahidi kufanya toba na wongofu wa ndani; kwa kujikita katika maisha ya kiroho na adili sanjari na kusimama kidete kupinga ukosefu wa haki.

Taasisi za elimu, shule na vyuo vikuu vina dhamana ya kudumisha amani, kwa kutoa malezi ya viongozi wa leo na kesho pamoja na kuleta mabadiliko muhimu katika taasisi za kiserikali kitaifa na kimataifa. Wafanye tafiti za ufumbuzi wa matatizo ya kiuchumi na kifedha kwa kuzingatia ut una tunu msingi za kimaadili. Wanasiasa wajitahidi kutafuta kwanza kabisa mafao ya wengi pamoja na kukuza ushirikiano na mshikamano kwa ajili ya ukuaji wa mtu binafsi na makundi kama msingi wa kweli wa elimu ya amani.

Baba Mtakatifu anaendelea kuhamasisha umuhimu wa kufundisha utamaduni wa amani kwa ajili ya mafao ya wengi, kwa njia ya mawazo, maneno, matendo na kwa kutimiza wajibu. Watu wajifunze kupendana, kuthaminiana na kuvumiliana. Wakatae tabia ya kulipiza kisasi na badala yake wakumbatie fadhila ya kusamehe wakipania kujenga msingi wa msamaha na upatanisho wa kweli. Amani ya kweli inajidhihirisha katika matendo, huruma, mshikamano, ujasiri na udumifu, kama anavyobainisha Yesu Kristo mwenyewe kwa njia ya maisha yake.

Ni mwaliko kwa kila mwamini kumwomba Mungu amwezeshe kuwa ni mjenzi wa amani; viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wajibidishe katika kutafuta amani kwa kubomoa kuta zinazowatengenanisha na kuimarisha kifungo cha upendo, uelewano, msamaha na udugu ili kweli amani iweze kutawala na kudumu.










All the contents on this site are copyrighted ©.