2012-12-29 12:22:12

Papa atuma salam za rambi rambi kutokana na kifo cha Mzee Matteo, Baba mzazi wa Kardinali Giovanni Battista Re


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumamosi tarehe 29 Desemba, 2012 amemtumia salam za rambi rambi Kardinali Giovanni Battista Re, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu baada ya kupatwa na msiba wa Baba yake mzazi Mzee Matteo Re aliyekuwa na umri wa miaka 104. Amefariki dunia hapo tarehe 27 Desemba 2012. Mazishi yamefanyika Jumamosi tarehe 29 Desemba 2012 na kuongozwa na Kardinali Battista Re.

Papa anatumia fursa hii kuwafariji wote walioguswa na msiba huu kwa kuwahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala hasa katika kipindi hiki cha maombolezo. Anamshukuru Mungu kwa ajili ya uwepo wa Mzee Matteo pamoja na mchango wake mkubwa kiasi kwamba, ameweza kuishi zaidi ya miaka mia moja, fursa ambayo imemwezesha kuona mengi.

Baba Mtakatifu anaiombea roho ya marehemu Mzee Matteo ili iweze kukutana na Hakimu mwenye haki na hatimaye kupata pumziko la milele, wakiwa na tumaini la uzima wa milele kutoka kwa Kristo mwenyewe. Anawapatia baraka zake za kitume, katika kipindi hiki cha maombolezo.







All the contents on this site are copyrighted ©.