Tafakari ya Neno la Mungu: Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu
Mpendwa mwana wa Mungu, leo tunasherehekea na kushangilia sherehe ya familia Takatifu.
Masiha amezaliwa ndani ya familia hii. Ndani ya familia hii kuna majukumu ya kutekeleza
ili mwana wa Mungu akae mahali stahili na kwa namna hiyo atufundisha namna ya kutenda
na kuishi kwenye familia zetu. Somo la kwanza
toka kitabu cha Hekima ya Yoshua bin Sira linaweka mbele yetu fahari na heri ya kuwaheshimu
wazazi na kuwatunza katika uzee wao. Heri ambazo ziko wazi kadiri ya somo hili ni
kuwa na uzao, na si uzao tu bali kufurahia uzao huo. Kuwa na maisha marefu na uzee
wa kusifika. Kwa kuwatunza wazazi na kuwapa heshima stahili mmoja afanya malipizi
ya dhambi zake.
Kwa hakika somo hili lasisitiza na kuweka mkazo juu ya amri
ya nne ya Mungu. Waheshimu baba na mama upate miaka mingi na heri duniani.
Mtakatifu
Paulo anapowaandikia Wakolosai anafafanua namna ya kuishi na kupendana katika familia.
Ameweka wazi fadhila ambazo zajenga maisha ya familia yaani, unyenyekevu, utu wema,
rehema na msamaha kwa kila mwanafamilia. Kilainisho cha fadhila hizi ni UPENDO kifungo
cha ukamilifu. Kama familia na hasa kila mwanafamilia ataweza kuitikia mwaliko huu
wa Mungu, basi familia nzima itakaa katika utulivu na amani ya kweli yaani inayokuza
mshikamano.
Mtume Paulo haishii tu kwenye upendo bila kuweka jambo la kutuweka
pamoja yaani kusikia na kusikiliza sauti ya Mungu kwa njia ya Neno la Mungu. Kwa kutafakari
Neno la Mungu tunajiweka tayari siku zote kukaa na Bwana aliye Neno wa Milele, aliye
Nuru angavu tuliyoipokea wakati wa siku ya Noeli.
Pamoja na fadhila nyingine
fadhila ya utii yatufaa kwanza kwa kutii Neno la Mungu na pili kutii mamlaka iliyowekwa
na Kristu katika familia. Baba ni mkuu wa familia yafaa kumtiii na kumheshimu lakini
yeye mwenyewe lazima aige mfano wa Kristo Mchungaji mwema anayewahangaikia kondoo
wake. Ndiyo kusema aoneshe daima fadhila ya upendo kwa mke wake, watoto wake na watu
wote .
Katika injili ya Luka tunapata mfano wa familia iliyo na utii kwa sheria
za kidini. Ni lazima wakampeleke mzaliwa wa kwanza hekaluni. Yesu Mwana wa Mungu atufundisha
kujitoa kabisa kwa Mungu anayetuagiza daima kutimiza mapenzi yake kwa njia ya Kanisa.
Kwa kumpeleka Yesu Kristo huko hekaluni wanaonesha pia wajibu wa kumwelisha mtoto
katika elimu ya dini na wajibu kijamii. Ndiyo kusema wewe mzazi unapaswa na unawajibika
kutoa mafundisho msingi ya kikristu na unawajibika kutafuta shule itakayomkuza mwanao
vema katika utu, ukristu na malezi kijamii.
Jambo jingine tunaloliona katika
Injili ni lile la Simeoni kumchukua mtoto Yesu toka mikono ya wazazi wake na baadaye
kumtoa kwa watu wote. Kwa jambo hili Simeon anawakilisha taifa la Israeli lililokuwa
likisubiri ujio wa Masiha na sasa amefika na kumtoa kwa wote maana yake Masiha si
wa Israeli tu bali ni kwa ajili ya mataifa. Simeoni katika maisha yake alikuwa akisubiri
bila manunguniko, ni alama ya wazee wa sasa ambao wanajikabidhi mikononi mwa Mungu
wakisali na kuimba daima na kungojea fadhili za Bwana huku wakitimiza wajibu wao wa
kujenga hekima katikati ya familia na watu.
Katikia injili pia kuna binti
mwanamke aitwaye Anna, huyu ni mfano wa unyenyekevu na uwajibikaji katika kutimiza
kazi ya Bwana. Ni mfano wa wale ambao wametayarisha njia ya Bwana na mapito yake.
Anatoka katika ukoo mdogo wa Asheri ambao mbele ya Waisraeli ni bure na maskini, lakini
toka hapo Anna anampokea Bwana kwa furaha. Hii ni habari ya furaha, kwako wewe mwamini
katika udogo wako na utauwa wako kuna matunda makubwa ya neema za Mungu.
Hawa
tuliowasikia katika Injili wakitenda kazi ya Bwana wanakuwa kichocheo cha wanafamilia
kutenda vema katika familia zao daima wakilenga utukufu wa Kristu uliokwishafunuliwa
kwetu na Bwana mwenyewe. Ninakutakieni heri tele wewe uliyemdau wa familia na hasa
unapoweka nguvu yako kukuza tunu bora za familia, ukiangazwa na Familia Takatifu ya
Yesu, Maria na Yosefu. Heri tena kwa jumuiya zote, parokia zote, mashirika ya kitawa
mliojiweka chini ya usimamizi na ulinzi wa familia takatifu.
Tumsifu Yesu Kristo
Maria na Yosefu. Tafakari hii inaletwa kwako na Pd. Richard Tiganya, C.PP.S.