2012-12-28 11:28:44

Padre Mkenda kufanyiwa Operesheni, Serikali Zanzibar yaahidi kuwasaka wahusika ili sheria iweze kushika mkondo wake!


Padre Ambrose Mkenda wa Jimbo Katoliki Zanzibar aliyepigwa risasi hivi karibuni anatarajiwa kufanyiwa operesheni kubwa, Ijumaa tarehe 28 Desemba 2012, ili kuondoa risasi mbili zilizoko mwilini mwake na kwamba, amevunjika taya, lakini anaendelea vyema, kadiri ya taarifa kutoka katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Madaktari wamekuwa wanaendelea na juhudi za kurekebisha taya lililovunjika baada ya Padre Ambrose Mkenda kupigwa risasi na watu wasiojulikana katika mkesha wa Siku kuu ya Noeli, katika eneo la Tomondo, nje kidogo ya mji wa Unguja, tukio ambalo limewasikitisha wapenda amani ndani na nje ya Tanzania.

Serikali ya Mapinzduzi Zanzibar imeahidi kutenda haki kwa kuhakikisha kwamba, watuhumiwa wanapatikana na kufikishwa kwenye mkondo wa sheria ili kujibu mashtaka. Hadi kufikia Ijumaa, tarehe 28 Desemba, 2012 hakuna mtu aliyekuwa amekwishakamata kuhusiana na tukio hili ambalo bado linaendelea kuacha maswali mengi yasiyokuwa na majibu! Hili ni tukio la pili kwa kutendwa dhidi ya viongozi wa kidini kwa siku za hivi karibuni Visiwani Zanzibar.







All the contents on this site are copyrighted ©.