2012-12-28 14:40:47

Maamuzi ya Baraza la Madaktari kuhusu madaktari waliogoma nchini Tanzania


Kutokana na mgomo wa madaktari uliotokea kati ya tarehe 23 na 29 mwezi Juni 2012.Wizara iliwasilisha malalamiko kwenye Baraza la Madaktari Tanganyika ili lifanye uchunguzi kuhusu madaktari hao.

Idadi ya madaktari wote waliogoma walikuwa 394, kati yao madaktari 376 walikuwa ni madaktari walio katika mafunzo kwa vitendo (Interns) kutoka hospitali za Muhimbili, K.C.M.C. Bugando, Mbeya Rufaa, St. Francis - Ifakara, Dodoma, Temeke, Mwananyamala, Amana, Haydom na Sekou Toure. Aidha, Madaktari waajiriwa (Registrar) 18 walishiriki katika mgomo huo kutoka hospitali ya Rufaa ya Mbeya.

Baraza lilipitia malalamiko yote na limetoa adhabu stahiki kwa kila daktari aliyethibitishwa kushiriki katika mgomo huo. Adhabu hizo zilikuwa katika makundi yafuatayo; onyo, onyo kali na kusimamishwa udaktari kwa muda wa kati ya mwezi mmoja na miezi sita.Vile vile kuna Madaktari ambao hawakuwa na hatia ya kushiriki katika mgomo na hivyo walifutiwa mashtaka.

MCHANGANUO WA ADHABU
·Waliofutiwa mashitaka madaktari 49
·Waliopewa onyo madaktari 223
·Waliopewa onyo kali madaktari 66
·Kusimamishwa kwa muda madaktari 30
·Mashitaka yaliyoahirishwa kutokana na wahusika kuhitaji ushauri wa kisheria madaktari 4
·Mashitaka yasiyosikilizwa kutokana na wahusika kutofika walipoitwa na Baraza madaktari 22

Wizara inakamilisha taratibu za kinidhamu kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma kwa Madaktari wote waajiriwa ambao walipatikana na hatia mbele ya Baraza la Madaktari. Wizara pia imeridhia kuwapa Madaktari waliokuwa katika mafunzo kwa vitendo fursa nyingine ya kuendelea na mafunzo hayo katika hospitali za Umma walizokuwepo kabla ya kuondolewa. Hata hivyo fursa hii haitawahusu Madaktari wote waliopewa adhabu za kusimamishwa na Baraza la Madaktari, hadi hapo watakapomaliza kutumikia adhabu zao.

HITIMISHO

Kwa taarifa hii madaktari wote waliofutiwa mashtaka na wale waliopewa onyo na onyo kali wanatakiwa kuwasilisha kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii barua kutoka kwa msajili wa Baraza la Madaktari ikithibitisha kurejeshewa usajili na kuruhusiwa kuendelea na mafunzo kwa vitendo. Vile vile madaktari waajiriwa (Registrar) wanatakiwa pia kuripoti kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya ili kupewa barua zao kulingana na Adhabu walizopewa.

Barua hizi zitatolewa kuanzia tarehe 2 Januari, 2013. Madaktari wote walio katika mafunzo kwa vitendo wanatakiwa kuanza kazi katika vituo vyao vya awali ifikapo tarehe 14 Januari, 2013.Hakuna muda utakaoongezwa kwa kipindi kilichobakia cha mafunzo kwa vitendo. Kwa wale wote waliopewa adhabu wataanza kutumikia adhabu hizo kuanzia tarehe ya adhabu hiyo ilivyotolewa.








All the contents on this site are copyrighted ©.