2012-12-27 08:24:26

Siku kuu ya Familia Takatifu iwe ni chachu ya kujikita katika malezi ya imani kwa watoto na vijana wa kizazi kipya!


Maadhimisho ya Siku kuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, sanjari na mwendelezo wa Mwaka wa Imani, iwe ni fursa makini kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, kujikita katika malezi ya imani kwa watoto wao, kwa kutambua kwamba, wazazi na walezi ni walimu wa kwanza wa Imani, Maadili na Utu wema. RealAudioMP3

Watoto wana haki na wajibu wa kuifahamu Imani kwa kina, ili waweze kuadhimisha vyema Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, sanjari na Jubilee ya miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Miaka 20 tangu Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki ilipochapishwa kwa mara ya kwanza na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili.

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linabainisha kwamba, Familia ni mahali pa kwanza kabisa pa kurithisha Imani, lakini kwa bahati mbaya, kwa sasa Familia nyingi zinakabiliana na changamoto, kinzani na vikwazo ambavyo vinazifanya Familia nyingi kushindwa kutekeleza wajibu na dhamana yake kwa Kanisa na Jamii. Watoto wengi wanashindwa kuonja na kushiriki maisha ya Kikristo kutoka ndani ya Familia zao.

Ndiyo maana Kanisa linaendelea kujipanga vyema zaidi kwa kuwahamasisha watoto wake kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya, katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Waamini watambue na kukumbuka kwamba, Familia inakabiliwa na changamoto pamoja na vizingiti vingi kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na athari za utandawazi, ambazo zinaendelea kubeza misingi bora ya maisha ya kiroho, kimaadili na kiutu kwa kukazia uhuru usiokuwa na mipaka wala kuwajibisha.

Maaskofu Katoliki wa Hispania wanasema kwamba, kuna haja kwa Familia za Kikristo kutoa kipaumbele cha kwanza katika kushiriki maisha ya Kisakrementi: kwa kuwa na maandalizi ya kina na endelevu kabla na baada ya kupokea Sakramenti mbali mbali za Kanisa, ili kuweza kuwa na moyo wa Ibadan a uchaji wakati wa maadhimisho haya kama walivyobainisha Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Familia liwe ni jukwaa ambalo wanafamilia wanalitumia kuungama Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na kuimwilisha katika uhalisia wa maisha, kwani Imani bila matendo hiyo imekufa ndani mwake. Kanisa linapenda kuwaona watoto wake wakiishi Imani tendaji inayojionesha katika matendo ya huruma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Imani ijioneshe katika kila hatua ya maisha ya mwanadamu, ili kuweza kuonesha shukrani kwa Mwenyezi Mungu kutokana na matendo yake makuu yanayojionesha hatua kwa hatua katika hija ya maisha ya binadamu; wakati wa raha na furaha; wakati wa magumu na machungu.

Maaskofu wanasema, kutokana na mwelekeo kama huu, Familia inakuwa ni mahali muafaka pa malezi ya kina kuhusiana na Imani, kwa kuwaonjesha watoto wao upendo wa dhati. Hii ni dhamana inayochangiwa na kuendelezwa na wadau wengine katika malezi yaani: walezi wengine, ndugu na jamaa; Parokia pamoja na Vyama vya Kitume.

Dunia ina kiu na njaa ya kuona na kuonja ushuhuda makini unaotolewa na Familia za Kikristo katika mchakato mzima wa kuyatakatifuza malimwengu na kukumbatia fadhila za maisha ya familia inayoangaziwa na mwanga wa Imani kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Kwa njia hii, Familia zitakuwa na uwezo wa kuhamasisha watu wengine kufungua akili na mioyo yao kwa ajili ya kumpokea Mwenyezi Mungu. Familia za Kikristo ziwe ni chachu ya utu wema na utakatifu wa maisha kwa Jamii inayowazunguka.








All the contents on this site are copyrighted ©.