Kanisa linamwimbia Mungu utenzi wa shukrani kwa Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50
ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican
Mama Kanisa anaendelea kumshukuru Mungu kwa wema na ukarimu ambao amelijalia katika
kipindi cha Mwaka 2012. Ni mwaka ambao umefumbata hija ya maisha ya kiimani inayomshirikisha
mwamini maisha na utume wa Yesu Kristo, aliyezaliwa, akateswa, akafa na kufufuka kutoka
katika wafu. Huu ndio msingi wa maadhimisho ya Mwaka wa Kanisa.
Ni sehemu ya
ujumbe wa Mheshimiwa Padre Dietrich Pendawazima, Makamu Mkuu wa Shirika la Waconsolata
Ulimwenguni, wakati akitoa salam na matashi mema kwa Familia ya Mungu popote pale
ilipo wakati huu wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli na Mwaka Mpya 2013.
Anasema,
kuzaliwa kwa Yesu Kristo kati ya watu wake, yaani Emmanuel, kunaonesha: imani na matumaini
ya watu wenye mapenzi mema, ambao wako tayari kumkaribisha Mwenyezi Mungu ili aweze
kuzaliwa tena katika maisha na vipaumbele vyao vya maisha. Ni changamoto endelevu
kwa waamini kumuungama, kumtangaza na kumshuhudia Kristo katika uhalisia wa maisha
yao, kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.
Maadhimisho ya Jubilee
ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican anasema Padre Pendawazima ni kati ya
zawadi kubwa ambazo Mwenyezi Mungu kwa njia ya Yesu Kristo amelizawadia Kanisa. Ni
Mtaguso ambao umekuwa ni dira na mwongozo kwa maisha na utume wa Kanisa katika Mapambazuko
ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Ni Mtaguso ambao umetoa msukumo wa pekee katika kumfahamu
Mungu aliyejifunua kwa njia ya Yesu Kristo; Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili.
Mtaguso
wa Pili wa Vatican una utajiri mkubwa ambao unapania kuwajengea uwezo waamini kushiriki
kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika misingi ya haki, amani,
upendo na mshikamano; kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene;
kwa pamoja wakitafuta mafao ya wengi; kwa kuheshimu na kuthamini utu wa mwanadamu
aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Waamini wanahamasishwa na Mababa wa
Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa,
kwa kumwilisha Neno la Mungu na Liturujia katika uhalisia wa maisha yao, kama njia
ya kuyatakatifuza malimwengu sanjari na kuendeleza kazi ya ukombozi iliyoanzishwa
na Kristo mwenyewe.
Padre Dietrich Pendawazima anasema, changamoto zilizotolewa
na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, uwawezeshe waamini kusoma alama za nyakati,
tayari kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa bila hata ya kujibakiza.