Watanzania kamwe msikubali kukumbatia utamaduni wa kifo! Dumisheni misingi ya haki,
amani na upendo!
Askofu mstaafu Mathias Joseph Issuja wa Jimbo Katoliki Dodoma anawataka watanzania
kupinga kwa nguvu zao zote sera za utoaji mimba pamoja na udhibiti wa ongezeko la
watu, kwani vitendo hivi ni kikyume kabisa cha mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu
aliyeumbwa kwa sura na mfano wake.
Askofu Issuja ameyasema hayo wakati wa mahubiri
katika Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2012, kwenye
Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba. Anawahimiza watanzania wakati huu wanapoendelea
kuchangia maoni yao kwenye Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba Mpya, kupinga ser na
mikakati inayopania kukumbatia utamaduni wa kifo.
Askofu Issuja amekazia kwa
namna ya pekee, umuhimu wa watanzania kuendelea kulinda, kutunza na kudumisha misingi
ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa, ili kuendeleza mafanikio yaliyokwisha
kupatikana nchini Tanzania kwa takribani miaka hamsini na moja iliyopita. Bila misingi
ya haki, amani na usawa, taifa linaweza kujikuta likitumbukia katika maafa. Amani
si bidhaa inayoweza kuuzwa au kununuliwa sokoni, bali ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi
Mungu inayowajibisha pia binadamu.
Maendeleo ya sayansi na teknolojia yasaidie
pia maboresho na uelewa wa watu wengi kuhusu hali yao ya maisha pamoja na kupambana
na hali mbali mbali kisayansi badala ya kuendekeza mila na desturi zilizopitwa na
wakati. Maendeleo na mafanikio yanapatikana kwa kufanya kazi kwa: bidii, juhudi na
maarifa na wala hakuna njia ya mkato kwa kukimbilia kwa waganga, matokeo yake ni mauaji
ya watu wasiokuwa na hatia, hali inayojenga hofu na wasi wasi miongoni mwa Jamii.
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yaimarishe imani, matumaini na mapendo katika Jamii
kama njia ya ushuhuda wa Imani katika matendo.