Ukweli na uwazi ni muhimu katika matumizi ya rasilimali ya Kanisa
Idara ya uchumi, fedha na mipango ya Vatican inapania kwa namna ya pekee, kuhakikisha
kwamba, shughuli zinazoendeshwa na Vatican katika masuala ya uchumi na fedha, zinazingatia
misingi ya ukweli na uwazi, kama ilivyobainishwa kwenye Taratibu Mpya zilizopitishwa
tarehe 22 Februari 2012 na kuanza kutumika hivi karibuni.
Hayo yamebainishwa
na Kardinali Giuseppe Versaldi pamoja na viongozi wengine waandamizi kutoka katika
Idara hiyo walipokuwa wanaelezea utekelezaji wa kanuni hizi ambazo kwa sasa zina mwelekeo
wa kimataifa. Ukweli na uwazi katika masuala ya fedha na uchumi ni mambo muhimu sana
katika maisha na utume wa Kanisa; ndani na nje ya Kanisa lenyewe. Mchakato huu unapania
pamoja na mambo mengine, kuimarisha uaminifu kwa Kanisa na utume wake ulimwenguni.
Idara
ya uchumi, fedha na mipango ya Vatican inasimamia, kuratibu na kudhibiti shughuli
zote za uchumi, fedha na mipango zinazoendeshwa mjini Vatican; mintarafu misingi ya
ukweli na uwazi. Licha ya kuwaamini watu wanaotekeleza wajibu na majukumu yao katika
masuala haya, lakini, hiki ni chambo cha juu kabisa cha kusimamia fedha na mali ya
Vatican.
Katika ulimwengu wa utandawazi, sayansi na teknolojia pamoja na athari
za myumbo wa uchumi kimataifa, Kanisa limejifunza kwa namna ya pekee kuhakikisha kuwa
linatumia vyema mchango unaotolewa na wafadhili mbali mbali kwa ajili ya kulitegemeza
Kanisa katika maisha na utume wake ulimwenguni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa
maskini na wahitaji zaidi.
Idara ya uchumi, fedha na mipango pamoja na mambo
mengine itakuwa na dhamana ya kuratibu na kudhibiti shughuli zote za uchumi na fedha
zinazofanywa na Vatican pamoja na vitengo vyake vyote, kama alivyokuwa amebainisha
Papa Paulo wa sita, kunako tarehe 15 Agosti 1967 alipokuwa anaanzisha Idara hii. Kwa
sasa Idara hii pia itajishughulisha na kupanga na kuelekeza shughuli mbali mbali zinazofanywa
na Vatican.
Askofu mkuu Vallejo Balda; katibu mkuu wa Idra ya uchumi, fedha
na mipango anasema, kwamba, makucha ya athari za myumbo wa uchumi kimataifa yameanza
kugusa hata uchumi wa Vatican. Kwa miaka kadhaa kwa sasa, mapato na matumizi ya Vatican
yamekuwa hayalingani, kwani kuna matumizi makubwa zaidi kuliko mapato ya Kanisa. Mchango
unaotolewa na Waamini pamoja na wafadhili mbali mbali haukidhi gharama za uendeshaji
wa shughuli na mikakati mbali mbali ya Vatican.
Sehemu kubwa ya mapato ya
Vatican yanaelekezwa zaidi kwenye mishahara ya wafanyakazi wake ambao kwa sasa wamefikia
elfu tano na mia tano. Ni fedha inayotumika kulipa pensheni na huduma za tiba.
Licha
ya mikakati mbali mbali inayotolewa ili kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli
za Vatican ili kuliwezesha Kanisa kuendelea kutoa huduma yake sehemu mbali mbali za
dunia; Vatican inapania kuhakikisha kwamba, rasilimali fedha na vitu vilivyopo vinatumika
barabara, na hasa zaidi kwa ajili ya kuwasaidia maskini na wahitaji zaidi, jambo ambalo
pengine halifahamiki na wengi au halijapewa uzito wa kutosha.