2012-12-25 15:02:59

Mashambulizi ya kijeshi yana athari kubwa kwa maisha ya watu na mali zao! Kuzeni utamaduni wa majadiliano, upendo na mshikamano!


Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum anasema, ni matumaini ya Kanisa kwamba, Jumuiya ya Kimataifa haitarudia tena makosa ya kufanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Syria, kama ilivyojitokeza nchini Iraq, Libia na Pwani ya Pembe kama suluhu ya kinzani na migogoro ya kivita iliyokuwa inaendelea katika nchi hizi.

Kardinali Sarah anasema, hija yake ya kichungaji aliyoifanya hivi karibuni nchini Lebanon kwa niaba ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, inaonesha kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza kwa vitendo maamuzi yao na waamini kwa upande wao wanapaswa kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kusali ili kuombea amani na utulivu katika nchi zao kwani amani, kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayotoa dhamana kwa binadamu kuendelea kuifanyia kazi.

Kardinali Sarah ameyasema haya mara tu baada ya Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, wakati Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alipomaliza kutoa ujumbe wake kwa mji wa Roma na Dunia kwa ujumla, unaojulikana kwa lugha ya Kilatini "Uribi et Orbi". Baba Mtakatifu amekazia pamoja na mambo mengine umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika misingi ya haki, amani, upendo na upatanisho wa kweli. Vita na mashambulizi yana athari kubwa kwa maisha na mali ya watu.

Umefika wakati anasema Kardinali Robert Sarah kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga utamaduni wa majadiliano ya kweli na kina! kama njia ya kutafuta suluhu ya kinzani, migogoro na vita inayoendelea kuibuka sehemu mbali mbali za dunia, kama alivyobainisha Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika ujumbe wake wakati wa Noeli.

Dunia imechoka kusikia mtutu wa bunduki ukirindima, ni maneno yaliyosemwa na Papa Paulo wa sita, yapata miaka hamsini iliyopita, yanaendelewa kurudiwa tena na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwani watu wanatamani kuona amani, usalama na utulivu vikitawala katika mioyo na kwenye viunga vya miji na vitongoji vyao.

Mama Kanisa hatakaa kimya na kuangalia vita ikiendelea kutokea sehemu mbali mbali za dunia, anawaalika waamini na wote wenye mapenzi mema anasema Kardinali Robert Sarah kuombea amani sanjari na kuendelea kusaidia wale wanaoathirika kutokana na migogoro ya kivita na kinzani za kijamii, kwani upendo na mshikamano wa dhati ni sehemu ya vinasaba vya Watoto wa Kanisa.







All the contents on this site are copyrighted ©.