Kanuni ya Imani ni muhtsari wa Imani, dira na mwongozo katika hija ya maisha ya waamini
hapa ulimwenguni
Waamini wanatakiwa kuwa watenda haki, wavumilivu, wastahimilivu na kuepuka kutumia
njia za mabavu na vitisho katika masuala mbalimbali ya kimaisha na kwamba hiyo ndiyo
neema pekee ya utashi itakayowafikisha mbinguni pamoja na kuendelea kuifanya dunia
kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Waamini wajikite katika maisha ya sala, tafakari
ya kina ya Neno la Mungu, matendo ya huruma, kama njia makini ya ushuhuda wa imani
yao kwa Kristo na Kanisa lake, wakati huu, dunia inaposhangilia kuzaliwa kwa Yesu
Kristo Mkombozi wa ulimwengu.
Hayo yamesemwa na Askofu Evaristo Chengula (IMC)
wa Jimbo Katoliki Mbeya wakati wa maadhimisho ya ibada ya misa takatifu ya mkesha
wa siku kuu ya noeli; kuzaliwa kwake Yesu Kristo iliyofanyika katika Kanisa kuu la
Mtakatifu Anthony wa Padua Parokia ya Mbeya Mjini Kuzaliwa kwake Yesu Kristo Mwana
wa Mungu; wakristo Wanapaswa kuutumia fursa ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kutafakari
tabia, kuthibitisha na kukiri imani na matumaini yaliyopandikizwa katika mioyo ya
waamini.
Aliwakumbusha kuwa Kanuni ya Imani inawataka Wakristo kusadiki kwa
Mungu mmoja hata kama mambo yanayojitokeza ni magumu na makubwa kuliko maumbile ya
mwanadamu huku unyenyekevu upole, haki na amani vikitawala. "Kristo alifauru katika
ukombozi wake wa dunia kwa sababu hakutumia mabavu katika maamuzi yake hadi walimuuwa
kwa hiyo imani yetu inakwenda kwa njia ya unyenyekevu, lakini kwa neema ya Mwenye
Mungu tunaweza kufauru katika kila jambo,"alisema.
Askofu Chengula alisema,
mara nyingi Kanisa lina mwono wa nguvu nguvu jambo ambalo Yesu Kristo anawakumbusha
kwamba, wanapaswa kuwa wanyenyekevu katika masuala mbalimbali hivyo, kujiunga na
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika kutolea ushuhuda wa Imani yao kwa
Kristo na Kanisa lake, kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Imani. "Wengi wanajifunza
na kusoma Biblia na Taalimungu lakini siyo wote wanaweza wakawa na imani siyo sababu
ya kusoma sana, bali ni neema na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kanuni ya imani
iwe ni kioo cha imani ya Kikristo, lazima tujiangalie sisi wenyewe kama kweli tunasadiki
na kufurahia imani hii kila siku na itawafanya wenye heri katika uzima ujao,"alisema.
Alisema
bila kuwa wenzi wa Roho Mtakatifu waimbaji hawataweza kuwashirikisha waamini kiasi
hata cha kuguswa na nyimbo zao licha ya kufanya kazi ya kitume kwani bila kuuwisha
na Roho Mtakatifu yote ni bure na mwisho wasio kuwa na Roho mtakatifu watabakia pembeni
kuwapisha wenye imani. Hata waumini wanaopanda mbele ya Altar kama hawana ndani mwao
Rho Mtakatifu masomo yao yataingia katika sikio la kulia na kutokea la kushoto, hayaingii
akilini mwake na kwa waumini na hivyo kuwa sawa na bure.
Askofu Chengula alisema
mwaka 2013 Jimbo Katoliki la Mbeya litafungua mchakato wa Sinodi ya Jimbo ambapo kila
mwamini atapaswa kutafakari baada ya programu kutolewa Januari,10,2013 katika siku
ya kuadhimisha Jubilee ya miaka 25 ya baadhi ya Mapadre Jimboni na baadaye itafuatia
utekelezaji wa maamuzi yaliyotolewa na Mababa wa Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu
wa Afrika, mintarafu vipaumbele vya Jimbo Katoliki Mbeya, Kanisa la Tanzania na Afrika
katika ujumla wake.
Katika Ibada ya Misa Takatifu, Askofu Chengula amebariki
na kuzindua Kinanda kipya kikubwa na ngoma kwa ajili ya kwaya ambavyo vimenunuliwa
kwa misaada ya waumini mbalimbali waliojitolea na amewashukuru waumini kuendelea kujitoa
kulichangia kanisa katika masuala mbalimbali na huo ndiyo utume.