Hotuba ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa wasaidizi wake wa karibu mwishoni
mwa mwaka, ni kati ya tafakari binafsi zinazoandaliwa kwa umakini mkubwa pamoja na
kuzama katika mada ambazo amezipatia kipaumbele cha kwanza, ili kuweza kushirikisha
mawazo kwa ujasiri mkubwa akitambua dhamana na wajibu wake kwa Kanisa na kwa Familia
ya binadamu katika ujumla wake.
Ni mawazo ambayo kwa kawaida yanakubalika,
lakini wakati mwingine yanapambana na upinzani mkubwa. Mwaka huu ameamua kuzungumzia
ukweli kuhusu Familia na Uwili unaoundwa kati ya Bwana na Bibi; Majadiliano na Utangazaji
wa Imani.
Padre Federico Lombardi katika tahariri yake anabainisha kwamba,
Baba Mtakatifu amechagua mada hizi, bila ya kugusia kuhusu miswada ya sheria, ndoa
za watu wa jinsia moja au maneno yaliyoonesha ukaribu wake wa pekee kwa Familia ambazo
zinakumbana na hali ngumu ya maisha wakati wa kesha la Maadhimisho ya Siku ya Familia
Kimataifa iliyofanyika Milano, Kaskazini mwa Italia.
Baba Mtakatifu anauliza
swali la msingi "mtu ni nani? Tofauti za kijinsia kati ya mwanaume na mwanamke ni
muhimu sana kwa utambulisho wa mwanadamu na uhusiano unaojengeka kati ya: baba, mama
na watoto ndani ya familia mintarafu mpango wa Mungu kwa mwanadamu.
Kukataa
uwepo wa tofauti hizi ni kukana ukweli na kutaka kuhalalisha kwamba, mwanadamu anaweza
kuchagua utambulisho wake mwenyewe, hali ambayo inapelekea kwenye mahangamizi ya utu
wa mtu! Mama Kanisa anaposimama kidete kutetea tunu msingi za maisha ya kifamilia
anamtetea mtu mwenyewe mintarafu ufahamu na mapokeo mbali mbali ya kidini.
Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anapopembua kuhusu majadiliano, Mkristo anaingia
katika Jukwaa hili kama mdau mkuu wa mang'amuzi ya maisha ya binadamu mintarafu mwanga
wa imani; akijitahidi kusimama kidete kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha adili
na kiutu licha ya kinzani zinazojitokeza.
Kanisa linajitosa uwanjani likiwa
na imani kwamba, tafiti za ukweli kamwe hazitahatarisha utambulisho wake, kwani si
kwamba mwanadamu anamiliki ukweli, bali anaongozwa taratibu ili kuweza kuufikia. Hii
ni dhamana pevu na nyeti na ni sehemu ya matashi mema ya kipindi cha Noeli, kuweza
kuzama zaidi ili kuangalia hali halisi ilivyo wakati huu.