Msimamo wa Kanisa kuhusu adhabu ya kifo unafafanuliwa vyema kwenye Katekisimu Mpya
ya Kanisa Katoliki
Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican amekanusha taarifa zilizotolewa na
baadhi ya vyombo vya habari kwamba, viongozi kadhaa wa Serikali ya Uganda wanaotembelea
Roma, walipokutana na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, mara baada ya Katekesi
yake siku ya Jumatano, tarehe 19 Desemba 2012 walipata baraka kwamba anaunga mkono
adhabu ya kifo kwa wale watakaopatikana na hatia ya kujihusisha na ndoa za watu wa
jinsia moja, jambo ambalo si kweli kabisa!
Padre Lombardi anasema, uvumi huu
unakwenda kinyume kabisa na mafundisho ya Kanisa na msimamo wa Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita kuhusu adhabu ya Kifo. Kusalimiana na mtu si tiketi ya kuhalalisha
sera za nchi husika. Rebeka Kadaga ni kati ya viongozi wa ngazi za juu kutoka Uganda
waliohudhuria Katekesi ya Baba Mtakatifu, Jumatano iliyopita na kwamba, binafsi anaunga
mkono adhabu ya kifo dhidi ya watu watakaopatikana na hatia hiyo.
Padre Lombardi
anabainisha kwamba, mafundisho ya Kanisa kuhusu adhabu ya Kifo yanafafanuliwa kwa
kina na mapana na Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki. Muswada wa sheria dhidi ndoa
za watu wa jinsia moja unaendelea kupingwa na watu mbali mbali ndani na nje ya Uganda.