2012-12-22 07:53:48

Mikakati ya shughuli za kichungaji nchini Senegal kwa Mwaka 2012-2017: Majadiliano ya kidini ili kujenga msingi wa haki, amani na mshikamano wa kitaifa!


Kardinali Thèodor Adrien Sarr wa Jimbo kuu la Dakar Senegal, hivi karibuni alizindua Mpango wa Shughuli za Kichungaji Nchini Senagal kwa Kipindi cha Miaka Mitano: 2013 – 2017. Maaskofu wanapenda kujikita zaidi katika majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam, kama njia ya kujenga amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. RealAudioMP3

Kwa upande wake, Familia ya Mungu nchini Senegal inapenda kutolea ushuhuda wa Imani yake kwa Kristo na Kanisa kwa njia ya huduma msingi za kijamii katika sekta ya afya, elimu na maendeleo endelevu. Wakristo wanatamani kuona kwamba, wanaishi miongoni mwa watu wanaopenda na kuthamini utamaduni wa amani; wakisaidiana katika shida na raha, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; tofauti zao za kidini, kiimani na hata mahali anapotoka mtu, kiwe ni kichocheo cha kutaka kukuza na kuimarisha amani, upendo na mshikamano kwa kuunda mazingira yatakayoiwezesha Senegal kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Senegal lilipata fursa ya kufanya tathmini ya kina kuhusu mipango na mikakati ya shughuli za kichungaji awamu ya kwanza na ya ile ya pili katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, yaani kuanzia mwaka 2000 hadi 2011. Katika mikakati yao, Maaskofu wanalenga zaidi: umoja, liturujia, ushuhuda na huduma makini kwa Familia ya Mungu nchini Senegal.

Kardinali Sarr anasikitika kuona kwamba, bado kuna vitendo vya choko choko dhidi ya Wakristo nchini Senegal kama ilivyojitokeza hivi karibuni kwa kunajisi makaburi ya Wakristo, vitendo ambavyo ni kinyume kabisa cha ubinadam na ustaarabu. Wakristo katika matukio kama haya, hawana budi kushinda kishawishi cha kutaka kulipiza kisasi na badala yake, waendelee kutumaini kwamba, Serikali itaweza kutekeleza wajibu wake kwa kuwatia mbaroni wahusika, kujibu tuhuma zinazowakabili. Serikali inawajibu wa kutoa ulinzi na usalama kwa raia na mali zao.








All the contents on this site are copyrighted ©.