Mheshimiwa Padre Estanislau Marques Chindekasse ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Dundo,
Angola
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita amemteua Mheshimiwa Padre Estanislau Marques
Chindekasse, SVD kuwa Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki la Dundo nchini Angola. Askofu
mteule alizaliwa tarehe 18 Agosti 1958, Huambo, Angola. Baada ya masomo na majiundo
yake ya Kikasisi, alipadrishwa tarehe 22 Novemba 1987. Tangu wakati huo ametekeleza
utume wake nchini DRC, Angola na Roma kwa ajili ya masomo ya juu alikojipatia shahada
ya Uzamivu katika Falsafa.
Jimbo Katoliki la Dundo lilizinduliwa kunako mwaka
2001 na sehemu ya Jimbo kuu la Saurimo. Kwa sasa lina jumla ya Parokia 7 zinazohudumiwa
na Mapadre 10: Kati yao kuna Mapadre watatu wa Jimbo na Mapadre wengine Saba ni kutoka
katika Mashirika ya Kitawa. Jimbo lina jumla ya watawa wa kike 17 na Waseminari 6.
Jimbo Katoliki Dundo lilikuwa wazi baada ya Askofu Josè Manuel Imbamba kuteuliwa kuwa
Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Saurimo.