2012-12-21 07:31:56

WCC: Kristo ni chemchemi ya uhai na maisha; ni mwanga wa watu wote!


Dr. Olav Fykse Tveit Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli anasema kwamba, Yesu anayekuja atawakirimia watu wa mataifa amani, mwanzi uliopondeka hauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli. Kristo ni chemchemi ya uhai na maisha ni mwanga wa watu wote. Yeye ndio ule mwanga unaoangaza giza na kamwe giza halitaweza kutawala. RealAudioMP3

Mzaburi analifananisha Neno la Mungu kama taa inayoangazia miguu ya watu wake, inayowaongoza katika safari ya maisha. Katika Maandiko Matakatifu kuna maelezo mbali mbali yanayochukua mwanga kuwa kama sura ya utukufu wa Mungu na maongozi yake. Wasanii kwa nyakati mbali mbali wameendelea kutumia picha hii katika Simulizi za kuzaliwa kwa Yesu Kristo; mwanga angavu unaoangaza kutoka mbinguni; ni mwanga wa Malaika unaoendelea kukua kutoka katika Pango ili kuweza kuzimulikia nyuso za binadamu.

Nabii Isaya anafundisha kwamba, Mtumishi wa Mungu hatauzima utambi unaofuka moshi ili kutoa mwanga katika giza. Mwanga huu utaendelea kung’ara licha ya uwepo wa giza, lakini kifo hakitamshinda Neno wa Mungu; Maisha na Mwanga wa Mungu. Neno ameleta maisha na uhai ni mwanga wa wote. Mwaka 2013 Baraza la Makanisa Ulimwenguni litajikita zaidi na zaidi katika ushuhuda na kazi mintarafu sala, kama sehemu ya mada itakayoongoza Mkutano mkuu wa kumi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni.

Mungu ni uhai na anawaongoza watu katika haki na amani. Kumbe, kipindi cha Majilio sanjari na Maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho, linaonesha kwa namna ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili anavyoendelea kukaa kati ya watu wake. Ni mwanga unaoleta matumaini katika ulimwengu mamboleo licha ya kinzani, nyanyaso, chuki, vita, uchoyo, rushwa na ufisadi.

Kristo ni Mwanga unaoiangazia miguu ya watu wake; anawaonesha watu njia ya haki na amani. Hata pale mwanga wa waamini unapoonekana kana kwamba, umefifia, Neno la Mungu litaendelea kuangaza na hatimaye, haki na amani vitapatikana.

Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anahitimisha ujumbe wake kwa Kipindi cha Noeli kwa Mwaka 2012, kwa kuwatakia kila la kheri na baraka wakati huu, Utukufu kwa Mungu juu na amani kwa watu wenye mapenzi mema.








All the contents on this site are copyrighted ©.