Ujumbe wa Noeli: tunataka viongozi wadhihirishe kwa vitendo: uadilifu, uaminifu, ukweli,
uzalendo na uchungu kwa nchi yao!
Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina wakati huu wa Kipindi cha Noeli, linasema katika
tafakari yake kwamba, wananchi wa Argentina wanahamu ya kusikia na kuonja kuwa, viongozi
nchini humo wanadhamiria kuonesha dira ya maendeleo endelevu kwa kudhihirisha kwa
matendo: uadilifu, uaminifu, ukweli, uzalendo na uchungu kwa nchi yao.
Viongozi wanaojifikiria
na kujitafuta wenyewe na kwa mafao yao binafsi hawana tena nafasi ya kupewa dhamana
ya kuiongoza nchi. Viongozi watafute kwanza kabisa mafao ya wengi.
Hii ni
tafakari ya kina iliyofikiwa na Maaskofu Katoliki Argentina mara baada ya mkutano
wa mia moja nan ne, uliojadili pamoja na mambo mengine Maadhimisho ya Mwaka wa Imani,
uliozinduliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.
Maaskofu
katika ujumbe wao, wanapenda kuwaelekezea zaidi viongozi ncghini Argentina kwamba,
wanayo dhamana kubwa nan yeti inayowakumbusha kwamba, watu bado wana imani kwamba,
wanaweza kujifunga kibwebwe kujenga nchi katika moyo wa udugu na mshikamano wa kitaifa.
Maaskofu
wanafanya upembuzi wa kina kuhusu hali halisi ya maisha ya wananchi wa Argentina ambao
wanakabiliana na mmong’onyoko wa maadili na utu wema; mambo ambayo yanagusa hata misingi
ya kitamaduni. Sheria za nchi hazina budi kuwalinda wanyonge badala ya kukumbatia
utamaduni wa kifo na athari zake zinazojionesha katika tunu bora za maisha ya kifamilia.
Kuna mwelekeo wa kutaka kutunga sheria zinazosigana na utu pamoja na heshima ya binadamu.
Mfumo wa elimu hauna budi kutoa nafasi kwa wazazi na walezi kuamua kuhusu
hatima ya watoto wao kwa siku za usoni, kwani wanatambua dhamana na utume wao katika
mchakato mzima wa malezi na makuzi ya watoto ndani ya Jamii. Kuna kundi kubwa la vijana
wa kizazi kipya linaonekana kukata tamaa na kukosa dira na matumaini kwa kesho iliyo
bora zaidi. Ni kundi ambalo wengi wao hawana hata nafasi ya kuendelea na masomo, kwani
kimsingi elimu ni ufunguo wa maisha.
Maaskofu wanasema kwamba, kuna ongezeko
kubwa la mtandao wa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya, hali ambayo inapelekea
ongezeko la vitendo vya jinai pamoja na ukosefu wa amani, usalama na utulivu kwa wananchi
wengi wa Argentina. Baada ya watu wengi kufurahia matunda ya demokrasia kwa takribani
kipindi cha miaka thelathini, kuna hatari kwamba, misingi ya demokrasia ikabomolewa
na hivyo kuweka vikwazo kwa watu wengi kushiriki katika masuala ya kisiasa nchini
humo.
Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli, Maaskofu wanasema, Argentina
inataka kuunda jukwaa la majadiliano, mahali pa kukutana na kujenga umoja na udugu;
watu wakiwa na dhamiri nyofu ya kutaka kuondokana na sera kandamizi, ubaguzi, chuki
na uhasama unaojengwa mioyoni mwa watu kwa mafao ya watu wachache ambao wamefilisika
kisiasa.
Nchi alimozaliwa mtu ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na
watu wanakabidhiwa kuiendeleza katika uhuru kamili. Licha ya matatizo, vikwazo na
changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo wananchi wa Argentina, lakini bado kuna
utashi mkubwa wa kutaka kujenga na kuimarisha umoja, udugu na mshikamano wa kitaifa.
Kila mtu akitekeleza wajibu wake, kwa hakika jambo hili linaweza kufanikiwa wanasema
Maaskofu Katoliki wa Argentina.