2012-12-21 09:37:48

Tanzania yafuzu kwa awamu nyingine kupatiwa
msaada wa fedha kutoka MCC


Tanzania ni miongoni mwa nchi tano zilizochaguliwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia, yaani Millenium Challenge Corporation (MCC) kwa ajili ya kupatiwa msaada wa fedha kwa awamu nyingine tena. Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Wakurugenzi ya MCC katika kikao chake kilichofanyika tarehe 19 Desemba, 2012 imebainisha majina ya nchi tano zenye sifa ya kupatiwa msaada huo wa fedha kutoka MCC na kuzitaja nchi hizo kuwa ni Tanzania, Liberia, Niger, Sierra Leone na Morocco.

Hivi sasa nchi hizo zinatakiwa kuandaa mapendekezo ya mipango yao ya maendeleo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, kwa ajili ya kupatiwa msaada wa fedha kwa awamu nyingine. Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji wa MCC, Bwana Daniel W. Yohannes, Tanzania na Morocco zimeendelea kufanya vizuri katika matumizi ya fedha za MCC zilizotolewa katika Awamu ya Kwanza na akabainisha kuwa nchi hizo zimekuwa washirika wazuri katika suala zima la utekelezaji.

Sifa za kupatiwa fedha kutoka MCC kwa awamu nyingine zinategemea utekelezaji mzuri wa mipango ya maendeleo inayojielekeza zaidi katika shughuli za kukuza uchumi na kupunguza umaskini.

Katika Awamu ya Kwanza, Tanzania ilipatiwa msaada wa fedha kutoka MCC wa jumla ya Dola za Marekani 698.1 milioni ambazo zimetumika katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo yenye lengo la kupunguza umaskini hapa nchini.








All the contents on this site are copyrighted ©.