2012-12-21 09:09:04

Salam za Noeli kwa Mwaka 2012 kutoka kwa Patriaki Fouad Twal


Patriak Fouad Twal wa Yerusalem katika ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2012; Mwaka wa Imani sanjari na Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican anayaangalia matukio mbali mbali yaliyojitokeza katika kipindi cha Mwaka 2012; mwaka ambao umekuwa ni chemchemi ya baraka, lakini pia kumekuwepo na machungu ambayo yamejitokeza katika hija ya maisha ya watu huko Mashariki ya Kati.

Kanisa limeendelea kudumisha majadiliano ya kiekumene na waamini wa madhehebu mbali mbali ya Kikristo kwa kuwataka kuendelea kuchangia katika ustawi na maendeleo ya nchi zao kwa kujikita zaidi na zaidi katika misingi ya haki, amani, ukweli, upatanisho na msamaha.

Juhudi hizi zinakwenda sanjari na majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam na Kiyahudi; viongozi wa kidini wanakumbushwa kwamba, wana dhana ya kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya amani na utulivu; kwa kuheshimiana na kuthaminiana pamoja na kuondoa mbegu ya chuki na uhasama kutoka katika mioyo ya vijana, juhudi ambazo zinapaswa kuanzia shuleni.

Kwa mara ya kwanza, hapo tarehe 5 Mei 2013 Makanisa ya Mashariki yataanza kuadhimisha kwa pamoja Siku kuu ya Pasaka, isipokuwa kwa Yerusalem na Bethlehemu mabadiliko haya yataanza kufanya kazi mwaka 2014. Waamini wa madhehebu na dini mbali mbali walihudhuria wakati wa kusimikwa kwa Papa Tawadros wa Pili mjini Cairo, kama kielelezo cha kuendeleza majadiliano ya kiekumene ili kujenga na kuimarisha umoja miongoni mwa Wakristo.

Patriaki Twal anasema, hali ya ulinzi na usalama huko Mashariki ya Kati bado ni tete, kiasi kwamba, inaweka wingu kubwa katika maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli kwa mwaka 2012. Kanisa linaendelea kuonesha mshikamano wake wa dhati kwa kuwapokea na kuwasaidia wakimbizi zaidi 250, 000 waliokimbia kutoka Syria na kwenda Yordani.

Azimio la Umoja wa Mataifa kuifanya Palestina kuwa ni kati ya nchi watazamaji wa kudumu wa Umoja wa Mataifa ni hatua ya kuridhisha katika mchakato wa kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu. Ni matumaini ya viongozi wa Kanisa kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itasaidia kuunda uwepo wa mataifa mawili yanayojitegemea. Kuna watu zaidi ya millioni moja na nusu wanaoishi katika Ukanda wa Ghaza, hali waliyo nayo inaonesha kwamba, bado wana chuki na hasira dhidi ya Israeli.

Kanisa bado linaendelea kuwasaidia wakimbizi ili kupata mahitaji yao msingi pamoja na kuhakikisha kwamba, sauti yao inasikika katika Jumuiya ya Kimataifa, hasa pale wanapokabiliana na mashambulizi yasiokuwa na msingi kama ilivyojitokeza hivi karibuni. Sekta ya elimu ni kati ya njia ambazo Kanisa linaendelea kutumia kama kielelezo cha majadiliano ya kidini na kiekumene; amani na utulivu miongoni mwa Jamii.

Patriaki Twal anawahimiza waamini Mashariki ya Kati kuendelea kujitajirisha kwa ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuhusu Kanisa Mashariki ya Kati, kama njia muafaka ya kuadhimisha Mwaka wa Imani. Mwishoni mwa mwezi Aprili 2013 kutafanyika mkutano wa kimataifa mjini Yerusalemu kuhusu maisha ya Papa Yohane wa Ishirini na tatu, muasisi wa Waraka wa Kichungaji kuhusu majadiliano ya kidini, Nostra Aetate; mkutano ambao unatarajiwa kuwashirikisha wasomi wa dini ya Kiyahudi.

Vijana kutoka Mashariki ya Kati wanatarajia pia kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013, huko Rio de Janeiro. Kipindi cha Noeli ni wakati muafaka wa kushirikishana na kumegeana furaha na shukrani kwa Mwenyezi Mungu na Watu wote wa Mungu popote pale walipo!







All the contents on this site are copyrighted ©.