Ninawaleteeni Habari Njema ya Wokovu: Uinjilishaji Mpya unaojikita katika chemchemi
ya furaha!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita pamoja na wasaidizi wake wa karibu, Ijumaa
tarehe 21 Desemba 2012 alishiriki katika tafakari ya tatu iliyoandaliwa na Padre Raniero
Cantalamessa, O.F.M.Cap. mhubiri wa nyumba ya Kipapa kama sehemu ya maandalizi ya
Siku kuu ya Noeli, kwa kujikita zaidi katika tema juu ya Uinjilishaji kielelezo cha
furaha ya ndani ya kukutana na Yesu Kristo, kama inavyojionesha pia katika Simulizi
za kuzaliwa Mtoto Yesu.
Hii ndiyo furaha ambayo Mzee Zakaria, Elizabeti, Bikira
Maria na wachungaji waliokuwa kondeni wakichunga mifugo yao waliionja kwa kusikia
Habari Njema ya kuzaliwa kwa Mkombozi wa dunia. Chemchemi ya furaha hii ni kutokana
na ukweli kwamba, Mwenyezi Mungu amewakumbuka na kuwatembelea watu wake, tayari kutekeleza
ahadi zake kwa wakati muafaka.
Padre Cantalamessa anasema kwamba, kuna haja
kwa waamini, baada ya kusikiliza Neno la Mungu kwa umakini katika Liturujia, kuendelea
kulimwilisha katika uhalisia wa maisha, kwa kushirikishana furaha hii kubwa ya kuzaliwa
kwa Mkombozi wa dunia, kwani hili ni tukio la kihistoria linaloacha chapa ya kudumu
katika maisha ya binadamu, kwa kutambua kuwa, Fumbo la Utatu Mtakatifu ndiyo chemchemi
ya furaha ya kweli.
Ni furaha inayoashilia mwanzo wa utekelezaji wa kazi ya
ukombozi, kama anavyobainisha Bikira Maria katika utenzi wake wa furaha kwa Mwenyezi
Mungu, ambaye aliuangalia unyonge wa mjakazi wake; wimbo ambao Mama Kanisa anaendelea
kuuimba kwa kumshukuru Mungu kwa matendo yake makuu aliyolikirimia Kanisa katika Kipindi
cha Karne ishirini zilizopita.
Mbegu ya ufalme wa Mungu inaendelea kukua na
kuchanua kutokana na neema na baraka mbali mbali zinazojionesha ndani ya Kanisa: kuna
umati mkubwa wa watakatifu, mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume na kwamba
licha ya mapungufu na ubinadamu unaojionesha ndani ya Kanisa, lakini nguvu za mauti
zimeshindwa kuliangamiza Kanisa la Kristo, kwa hakika hiki ni kielelezo cha uwepo
endelevu na utendaji wa Mungu ndani ya Kanisa.
Furaha ya kweli iwe ni mchakato
wa toba na wongofu wa ndani, kwa kutambua na kukiri mapungufu yaliyojionesha miongoni
mwa Watoto wa Kanisa, tayari kuomba msamaha na kuanza hija inayoelekea kwenye Utakatifu
wa Maisha. Waamini wajikite katika tafakari ya kina ya Neno la Mungu, wajitoe kimasomaso
kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao; wakionesha mshikamano
wa huruma na upendo kwa wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kanisa lijitahidi
kujenga na kuimarisha umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Licha ya furaha,
lakini mwanadamu anaendelea kukumbana na mazingira yanayoashilia huzuni na mahangaiko,
kiasi cha kudhani kwamba, hakuna Mungu, hali inayopelekea watu wengi kukengeuka na
kutopea katika malimwengu; matumizi haramu ya dawa za kulevya, mauaji ya kutisha yanayoendelea
kutawala katika vyombo vya habari, mmong'onyoko wa maadili na utu wema; ni kati ya
mambo ambayo yanamvunja moyo mwanadamu wa leo.
Lakini, waamini wasisahau kwamba,
licha ya furaha kubwa iliyoletwa na Habari Njema ya Wokovu, kilele chake ni Fumbo
la Msalaba; yaani mateso, kifo na ufufuko wake! Ushindi wa kishindo kuelekea maisha
ya uzima wa milele. Mwenyezi Mungu ni mwanga unaoyaangazia mapito ya mwanadamu usiku
na mchana; matumaini ambayo kamwe hayawezi kudanganya!
Ni furaha inayobubujika
kutoka katika undani wa mtu, kwa kumkirimia amani na uwezo wa kupenda na kupendwa;
Yesu Kristo ni bandari salama, changamoto kwa waamini kumtolea ushuhuda wa furaha
na matumaini ya kweli; huruma na msamaha pamoja na kupokea kila hali ya maisha kwa
imani na matumaini.
Ni Mwaliko wa kuendeleza majadiliano na ulimwengu na kuwa
na mawazo na mwelekeo chanya! Watoto wa Kanisa waoneshe furaha, amani na utulivu sanjari
na kuendelea kuwafariji wote wanaoteseka kiroho na kimwili, kwani furaha ya Kristo
ndiyo nguvu yao!