"Msizime kamwe moto wa matumaini licha ya ugumu na ukata wa maisha"
Kardinali Angelo Scola, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano, Italia, amewaandikia waamini
na watu wenye mapenzi mema Jimboni mwake, kutozima kamwe mwanga wa matumaini, licha
ya magumu na changamoto nyingi wanazoendelea kukabiliana nazo katika hija ya maisha
yao ya kila siku, kwa kutambua kwamba, Yesu Kristo anaendelea kuandamana nao katika
safari yao ya maisha.
Ni mwaliko
na changamoto ya kumkaribisha Kristo katika uhalisia wa maisha yao, wakiwa na imani
na matumaini kwamba, kamwe, hawako peke yao! Kwa namna ya pekee, anapenda kuwakumbuka
watoto, wazee, wagonjwa na wote ambao wako katika uvuli wa mauti bila kuwasahau wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa.
Kardinali
Scola anawaandikia watoto Jimboni mwake, akitaka waandamane naye katika hija ya kumtafuta
na hatimaye kumwona Mtoto Yesu anayezaliwa kwa mara nyingine tena katika maisha yao.
Noeli, Kanisa linafanya sherehe ya kuzaliwa kwa Mtoto Yesu, Mwana wa Mungu. Hii ndiyo
zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu anapenda kumzawadia kila mwanadamu. Zawadi zote
ambazo watoto hao watapokea wakati wa sherehe za Noeli ni kielelezo cha ujio wake
kati yao!
Kardinali Scola anawakumbuka wagonjwa na wote walioko kufani, katika
shida na mahangaiko yao ya ndani, watambue kwamba, kwa hakika Mwenyezi Mungu yuko
pamoja nao, kama walivyo wazazi kwa watoto wao. Hii ndiyo Habari Njema ya Wokovu katika
kipindi cha Noeli kwa Mwaka 2012.