2012-12-21 16:18:37

Mapigano kati ya wakulima na wafugaji yapelekea watu 30 kupoteza maisha nchini Kenya


Zaidi ya watu thelathini wamepoteza maisha kutokana na mapigano ya kikabila kati ya watu kutoka kabila la Pokomo na wale wa kabila la Orma Wilayani Mto Tana, nchini Kenya. Choko choko za makabila haya mawili ya wakulima na wafugaji zinatokana na kugombea mahali pa kulishia mifugo dhidi ya wakulima pamoja na mahali pa kunyweshea mifugo yao, hali ambayo wakati mwingine imesababisha uharibifu mkubwa wa mashamba ya wakulima.

Mapigano kati ya wakulima na wafugaji kati ya Mwezi Agosti na Septemba 2012 yalipelekea watu zaidi ya mia moja na kumi kupoteza maisha yao. Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya ameitaka Serikali kuhakikisha kwamba inachukua hatua madhubuti ili kuokoa maisha ya watu wasiokuwa na hatia pamoja na kutafuta chanzo kikuu kinachopelekea mapigano ya kikabila nchini Kenya, ili tiba muafaka iweze kupatikana, watu waishi kwa amani na utulivu.

Kuzagaa kwa silaha za moto ni kati ya mambo yanaopelekea mauaji ya watu wengi wakati wa mapambano kati ya wakulima na wafugaji. Wachunguzi wa masuala ya kiasiasa wanabainisha kwamba, kuna baadhi ya wanasiasa wanatumia kinzani na migogoro ya kikabila kwa ajili ya kujijenga kisiasa!







All the contents on this site are copyrighted ©.