2012-12-20 08:26:03

Watanzania wanahamasishwa kuchangia katika kujiletea maendeleo yao wenyewe! Serikali itasaidia kuona juhudi hizi zinazaa matunda yanayokusudiwa!


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda ameahidi kuchangia gharama za ununuzi wa jenereta kwa ajili ya kata ya Majimoto wilayani Mlele mkoani Katavi ili waweze kuwa na umeme wa uhakika. Alitoa ahadi hiyo Jumatano, Desemba 19, 2012 wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Majimoto kwenye uwanja wa mpira akiwa katika siku ya saba ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi.

“Kuna wafanyabiashara wa hapa Majimoto ambao walikuja kuniona na wakasema wako tayari kuchangia ununuzi wa jenereta lenye uwezo wa kutoa kilovoti 60 za umeme kwa nyumba kama 300. Wao watoe milioni 25 wakiwa tayari na mimi nitatoa milioni 25... jaribuni mkae na kupanga namna ya kuchangia gharama.” “Baada ya muda fulani mtakuta mmemaliza kuchangia, tuwarudishie wafanyabiashara hela yao ili hilo jenereta liwe la kijiji. Mkilipata, nitawasiliana na TANESCO ili watupatie nguzo za umeme,” alisema.

Akijibu hoja kuhusu viwanja, Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa Jimbo la Katavi alisema upimaji wa viwanja ulifanyika miaka miwili iliyopita na vikapatikana viwanja 270 lakini hadi sasa havijagawiwa kwa wananchi. Aliwataka viongozi wa kata na wilaya wasimamie zoezi hilo. Hata hivyo, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaonya juu ya ujenzi wa nyumba za makazi na biashara kando ya barabara kuu. ” Ninawasihi sana mheshimu sheria za barabara... msijenge nyumba zenu ndani ya hifadhi ya barabara.

Wakati huo huo, Waziri mkuu Mizengo Pinda ameahidi kutoa mizinga ya nyuki 25 ya kisasa na ya kibiashara kwa ajili ya Kikundi cha Sanaa cha kata ya Mamba wilayani Mlele mkoani Katavi ili waweze kuzalisha mali na kujiendesha wenyewe. Alitoa ahadi hiyo Jumatano, Desemba 19, 2012 wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Mamba kwenye uwanja wa mpira akiwa katika siku ya saba ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi.

“Nitawapa mizinga 25 ya kuanzia ili muongeze na ile miwili mliyopewa na Dk. Kikwembe (Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Katavi)... nataka ninyi muwe chachu ya mabadiliko hapa mamba ili vijana wengine na wazee waige kutoka kwenu,” alisema. Aliwataka wabadili mtazamo wao katika kufuga nyuki kwa kuweka mizinga ardhini au kwenye mabanda badala ya kuitundika kwenye miti. “Mnapaswa kufuga kisasa ili muweze kuikagua mara kwa mara, sasa ukiitundika juu ya mti utaendaje kuchungulia kama nyuki wameingia kwenye mzinga au la? Utajuaje kama masega yaliyomo yana asali ya kutosha? Alihoji.

Alisema wanapaswa watambue kwamba nyuki anafugwa kama ilivyo kwa viumbe wengine kama vile kuku, mbuzi, bata au ng’ombe. “Faida mtakayopata hapa ni kuwa karibu na msitu wa Lyamba lya Mfipa. Tungeweka mizinga pale chini ya msitu jioni hii, kesho asubuhi mngekuta nyuki wameshaingia na kuanza kazi,” aliongeza.










All the contents on this site are copyrighted ©.