2012-12-20 09:16:33

Wahudumu wa sekta ya afya ni wajumbe wa furaha na matumaini kwa wagonjwa na maskini


Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, Jumatano tarehe 19 Desemba, 2012 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wafanyakazi wa sekta ya afya mjini Roma, Ibada iliyofanyika kwenye Kanisa la Santo Spirito in Sassia.

Katika mahubiri yake amekumbusha kwamba, Mama Kanisa katika kipindi hiki maalum kuelekea maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho, yaani Siku kuu ya Noeli anaonesha utajiri mkubwa wa Liturujia ya Neno la Mungu unaofumbata Mpango wa Mungu katika kazi ya Ukombozi.

Mwenyezi Mungu ameonesha huruma na upendo mkuu, akawaandaa na kuwatuma Manabii kwa nyakati mbali mbali ili kumwandalia njia Mwanaye Mpendwa. Utukufu wa Mungu umejionesha kwa namna ya pekee kwa maskini na wanyonge, wale waliokuwa wanabezwa na kudharauliwa na Jamii.

Ili kuweza kumpokea Mungu anayewatembelea waja wake, kuna haja ya kuwa na imani na matumaini thabiti kama alivyoonesha Elizabeth; ukosefu wa imani una gharama zake, kama ilivyomtokea Mzee Zakaria alipotia shaka kuhusu mpango wa Mungu katika maisha na familia yake. Fundisho kuu linalojitokeza hapa ni kuhusu umuhimu wa Sala hasa wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Waamini wajifunze kusali vyema na kamwe wasijikatie tamaa na kulegea katika sala. Sala ya Baba Yetu ni muhtasari wa Mafundisho Makuu ya Yesu na ni sala ya Kikristo.

Waamini watambue kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda, anawasikiliza na kuwakirimia katika mahitaji yao hata kama si kama walivyoomba, kwani Yeye ni mwingi wa huruma na mapendo kwa wote wanaokimbilia kwake. Ulimwengu mamboleo unawahitaji wajumbe watakaotangaza furaha, amani na matumaini kama alivyofanya Yohane Mbatizaji, hasa kutokana na ukweli kwamba, kuna watu wamekata tamaa kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, hawana tena matumaini ya kesho iliyo bora zaidi.

Askofu mkuu Zimowski anawaalika wafanyakazi katika sekta ya afya kuwa ni wajumbe na mashahidi wa huduma ya upendo na mshikamano kwa wagonjwa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, kama walivyofanya watakatifu Filippo Neri na Mtakatifu Camillo wa Lellis. Ni watakatifu waliowapokea, wakarimu na kuwatibu wagonjwa, maskini na mahujaji mbali mbali waliokuwa wanatembelea Roma. Huu ndio wajibu msingi hata kwa wahudumu wa Sekta ya Afya wanaopaswa kutekeleza huduma hii wakisukumwa na upendo wa Kristo unaowawawajibisha katika utekelezaji wa majukumu na dhamana ya huduma kwa wagonjwa.

Athari za myumbo wa uchumi kimataifa zinaanza kuonesha pia makucha yake katika sekta ya afya kwani Serikali nyingi zinaanza kupunguza bajeti na ruzuku kwa Hospitali kama njia ya kubana matumizi, lakini zinasahau kwamba, waathirika wakuu ni wagonjwa na familia zao. Hospitali akama anavyosema Baba Mtakatifu ni Jukwaa la Huduma na Uinjilishaji Mpya, hapa wagonjwa wanapaswa kukutana na Wasamaria wema wanaowahudumia kiroho na kimwili.

Kuna haja ya kuwa na huduma makini, sawa na zinazozingatia utu na heshima ya mwanadamu; maadili, sheria na kanuni za afya. Upendo kwa Mungu na jirani, kiwe ni kipimo cha huduma kwa wagonjwa na maskini; kwa njia hii wafanyakazi hawa watakuwa wanasaidia kutekeleza mchakato unaopania kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, kwa kutumia hata ile rasilimali kidogo iliyopo kwa ajili ya mafao ya wengi.

Askofu mkuu Zygmunt Zimowisk anahitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli yawe ni kikolezo cha kuwamegea jirani furaha na matumaini, kwa kutambua kwamba, hata wahudumu wa Sekta ya Afya ni wadau wakuu wa dhamana ya Uinjilishaji Mpya, wanaochangia katika mapambano dhidi ya maradhi duniani.







All the contents on this site are copyrighted ©.