2012-12-20 07:42:15

Uinjilishaji Mpya ni utume unaovaliwa njuga na Mama Kanisa wakati huu!


Mwanadamu amekirimiwa na Mwenyezi Mungu uwezo wa kusikiliza kwa makini na hatimaye kutambua ujumbe unaokusudiwa kwake. Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uwasaidie waamini kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini Neno la Mungu, taa inayoangazia mapito ya maisha yao. Mama Kanisa anatambua umuhimu wa Uinjilishaji Mpya, dhamana ambayo inafanyiwa kazi katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. RealAudioMP3

Lakini kwa bahati mbaya, Ulimwengu unaonekana kana kwamba, umepoteza ile hamu na uwezo wake wa kusikiliza. Mwanadamu hapendi tena kusikia habari kuhusu Mwenyezi Mungu, wanataka hata kumwondoa katika maisha na vipaumbele vyao! Ni mtu aliyekengeuka anayependa kukumbatia utamaduni wa kifo; Familia kwake, haina thamani tena; kazi si kipimo cha utu na ukamilifu wa mwanadamu, bali bidhaa inayoweza kuuzwa na kununuliwa sokoni; uchumi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ndizo mada zinazopamba masikio ya mwanadamu katika ulimwengu wa utandawazi.

Watu hawajisikii tena kujenga na kudumisha uhusiano wa kweli na wa dhati, kwani wanaogopa kuwajibika. Kwa hakika, ulimwengu unahitaji maneno yanayotibu na kuponya! Mwanadamu anahitaji neno la matumaini ili kuvunja kimya kinachoendelea kutawala katika maisha ya mwanadamu hata pengine ndani ya Kanisa lenyewe!

Hii ni sehemu ya barua ya kichungaji kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Malta wakati huu wa Kipindi cha Majilio, Mama Kanisa anaposubiri kwa hamu kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mkombozi wa Ulimwengu. Neno linaloponya na kumrudishia mwanadamu uwezo wake wa kusikia na kuwasiliana na wengine ni Habari Njema ya Wokovu, Injili ambayo ni Kristo mwenyewe!

Mwenyezi Mungu anaipenda dunia, ndiyo maana amemtuma Mwanaye Mpendwa yesu Kristo, aje kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Yesu ni Neno linaloponya! Watu wanahamu ya kukutana na Yesu Kristo anayewapatia maana ya maisha, amani na utulivu wa ndani; anawakirimia furaha na matumaini.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anasema, hiki ndicho kiini cha Uinjilishaji Mpya, unaopania kumwonesha mwamini upya wa kukutana na Yesu, licha ya pilika pilika na changamoto za maisha katika ulimwengu wa utandawazi. Huu ndio utume unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa, Ole wake, kama Kanisa litashindwa kufanya hivi.

Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Neno la Mungu linapenya hadi kugusa moyo wa mwanadamu, dhamana inatìyohitaji kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mikakati na shughuli za kichungaji.

Waamini wachangamkie usomaji, tafakari na umwilishaji wa Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha na vipaumbele vyao. Ni mwaliko wa kuendeleza majadiliano ya kina, kwani kwa njia hii, watu wanaweza kuguswa na uwepo wa Mungu katika hija ya maisha yao! Imani katika Yesu inaponya, kama inavyojionesha katika matukio mbali mbali kwenye Maandiko Matakatifu; lakini jambo la msingi ni kuanzisha mchakato wa majadiliano na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sala!

Kanisa halina budi kujibu kilio cha watu wanaoendelea kuelemewa na uzito wa Misalaba yao ya maisha. Ni watu ambao wamejeruhiwa: kimaadili, kiutu na kiimani. Kama yule Msamaria mwema, Kanisa halina budi kuwapatia tiba ya kweli kwa njia ya Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti. Kanisa liendelee kufanya hija na wote wanaoteseka na kudhulumiwa, waliojeruhiwa, ili aweze kuwagusa na kuwaponya katika shida na mahangaiko yao.

Katika dhamana ya Uinjilishaji Mpya, Mama Kanisa anapenda kupangusa machozi ya wale wanaolia na pale inapowezekana kuzuia kabisa machozi haya yasimwagike! Uinjilishaji Mpya hauna budi kujikita katika maisha ya mwanadamu kwa kuanzia kwenye: familia, maeneo ya kazi, urafiki, umaskini pamoja na majaribu mbali mbali ya maisha.

Baraza la Maaskofu Katoliki Malta linasema kwamba, hakuna Uinjilishaji Mpya pasi na toba na wongofu wa ndani, ili kuchuchumilia utakatifu wa maisha. Dhamana hii inawezekana pale tu, waamini watakapoonesha moyo wa toba, ili kufungua masikio ya mioyo yao, kusikiliza kwa umakini Neno la Mungu na kupokea nguvu ya Kristo inayoponya!

Kipindi cha Majilio na hatimaye, Noeli ni Maandalizi ya Ujio wa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, kwa njia ya Roho Mtakatifu, na kukaa tumboni mwa Bikira Maria, nyota ya Uinjilishaji Mpya. Alisaidie Kanisa kutekeleza wajibu pamoja na kukabiliana na changamoto mbali mbali katika azma ya Uinjilishaji Mpya, ili viziwi waweze kusikia Habari Njema ya Wokovu na Bubu waweze kutangaza utukufu na matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu!








All the contents on this site are copyrighted ©.