2012-12-20 07:33:12

Familia ya Mungu Ghana katika huduma ya Upatanisho, haki na amani!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana katika mkutano wao wa Mwaka uliohitimishwa hivi karibuni wanabainisha kwamba, haki ni fadhila ya kwanza kabisa ambayo inapaswa kutolewa na taasisi mbali mbali ili kujenga na kuimarisha misingi ya upendo na amani. RealAudioMP3

Hakuna amani inayoweza kupatikana pasi na kuzingatia misingi ya haki na kwamba, haki ni matunda ya upatanisho wa kweli kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake wa kichungaji, “Africae Munus”, “Dhamana ya Afrika”. Mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana kwa mwaka 2012 uliongozwa na kauli mbiu “Familia ya Mungu katika huduma ya upatanisho, haki na amani.

Maaskofu Katoliki Ghana wanabainisha kwamba, matunda ya haki na upatanisho ni amani inayopata chimbuko lake katika undani wa maisha ya mwanadamu na matunda yake kusambaa ndani ya Familia na Jamii kwa ujumla. Kanisa kama Familia ya Mungu inao utume wa kuwa ni chombo cha upatanisho, haki na amani katika Jami husika. Ghana wanasema Maaskofu ni Familia ya Mungu na kwamba, Familia ni kitovu cha umoja miongoni mwa Jamii, changamoto ya kuvuka vikwazo vya kikabila na kikoo na hivyo kujisikia kuwa ni watu wa Familia moja ya Mungu inayowajibika.

Mwelekeo huu uwawezeshe wananchi wa Ghana kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa chini ya uongozi wa Rais wao kama mkuu wa Familia ya Ghana. Lakini pia wanawahimiza wanasiasa kutekeleza vyema wajibu na majukumu yao, wakitambua na kuthamini wajibu waliokabidhiwa na Familia kubwa ya wananchi wa Ghana katika hija ya maisha yao. Watambue kuwa, uongozi halali unatoka kwa Mwenyezi Mungu, unapaswa kujikita kwa ajili ya kutafuta mafao ya wengi. Serikali ya Ghana iendelee kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho.

Katika mkutano wao wa Mwaka, Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana limejadili pamoja na mambo mengine kuhusu: mikakati ya shughuli za kichungaji, hali ya kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa kutambua kwamba, kuna haja ya kuendeleza mipango ya maendeleo iliyokwisha kubuniwa na viongozi mbali mbali, ili kuwawezesha wananchi kufaidi matunda ya kazi hii kubwa. Ghana inapaswa sasa kujielekeza katika kuanza mchakato wa kufanya marekebisho makubwa katika Katiba ya Nchi.

Wameangalia pia uhusiano kati ya Kanisa na Serikali katika sekta ya elimu. Kwa namna ya pekee, wamehimiza umuhimu wa kuwa na uhuru wa kuabudu mashuleni; mustakabali wa watu wenye kipato cha chini Ghana; mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi; ulinzi nau salama. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu kwamba, viongozi wa Serikali watawajibika kikamilifu kulinda na kutunza mali ya umma; kwa kuzingatia misingi ya ukweli, uwazi na uzalendo kwa nchi yao.








All the contents on this site are copyrighted ©.