Familia ni kitalu cha miito mitakatifu, kamwe waamini wasiwe ni kikwazo cha Mapadre
wakaanguka na kugeuka kuwa mnara wa chumvi!
Askofu mkuu Yuda Thadeus Ruwaichi wa Jimbo Kuu la Mwanza, Tanzania katika Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani, ametusaidia kutafakari kuhusu utume wa Nabii, dhamana na wito wa
kipadre, leo katika makala haya anapembua utume wa Familia ya Kikristo katika kulea,
kukuza na kuimarisha wito wa Kipadre.
Askofu mkuu
Ruwaichi anasema kwamba, Padre ni baba wa Kanisa. Wazazi baada ya kuhangaika naye
katika malezi na majiundo na hatimaye kulikabidhi Kanisa, wanapaswa kumruhusu mtoto
wao ili aweze kuijenga nyumba yake, yaani Kanisa analokabidhiwa na kamwe huu usiwe
ni mradi binafsi au kitega uchumi kwa Familia, Ndugu, Jamaa na Marafiki, vinginevyo
atakuwa ni Padre asiye na raha na amani; asiye aminika wale kuheshimika kwani watu
wengi watadhani kwamba, anatumia Kanisa kwa ajili ya kuwafaidisha ndugu zake tu!
Wazazi
wanapaswa kutambua kwamba, mwana wao ni Padre wa Kanisa lote: Moja, Takatifu, Katoliki
na la Mitume. Idadi ya Mapadre inayoongezeka kila mwaka majimboni inuie kukuza ubora
na thamani na ufuasi wa Kristo; wakipania kumtangaza Kristo kwa njia bora zaidi, mpya,
hai na endelevu. Ni wajibu wa Familia ya Mungu kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea
miitomitakatifu ndani ya Kanisa, ili Kristo aweze kujipatia vijana wachapakazi, wachamungu
na hodari, tayari kujitoa kimaso maso, kumtangaza, kumpenda Kristo aliyeteswa, akafa
na kufufuka kutoka katika wafu.
Askofu mkuu Ruwaichi anazitaka Familia kuweka
nia wazi na thabiti ya kuboresha vitalu vya miito mitakatifu, kwani kila kuhani ni
tunda la Familia. Miito mizuri na dumifu ni matokeo ya Familia imara, zenye imani
thabiti, mshikamano, amani na upendo. Ni Familia ambazo ziko tayari kurithisha imani
na kulea maadili bora, kwa kutambua kwamba, Familia ni kitalu cha kuzalisha miito
mitakatifu na kamwe waamini walei wasiwe ni kikwazo cha kuanguka kwa Mapadre kwa kuwafanya
wageuke na kuwa ni minara ya chumvi!
Askofu mkuu Ruwaichi anawakumbusha Mapadre
kwamba, wanapoitikia wito kutoka kwa Mungu, wafanye hivyo kwa nia safi na wawe tayari
kuitikia kila siku ya maisha yao; katika raha, na furaha; magumu na shida na kamwe
wasijutie kuwa Mapadre, bali wawe imara na watakatifu!