2012-12-19 09:29:30

Tafuteni mikakati ya kuimarisha ujenzi wa misingi ya amani na utulivu kati ya Waislam na Wakristo Barani Afrika


Makamu wa Rais wa Tanzania Dr. Mohamed Gharib Bilal, amewataka wasomi wa dini ya Kiislam kutoka sehemu mbali mbali Barani Afrika kuhakikisha kwamba, wanawekeza katika elimu dunia kama sehemu ya urithi kwa watoto na vijana wa kizazi kipya ili kupambana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, sanjari na kulinda pamoja na kudumisha misingi ya amani na utulivu.

Dr. Bilal ameyasema hayo tarehe 17 Desemba 2012 wakati akifungua semina ya siku tatu ya wasomi wa dini ya Kiislam kutoka katika nchi mbali mbali Barani Afrika. Elimu ni njia pekee itakayoweza kurekebisha mwono potofu kwamba, waamini wa dini ya Kiislam ni watu wanaosababisha vurugu na kinzani katika Jamii. Watoto wafundishwe masuala yanayogusa maisha ya kiroho, uvumilivu na uelewano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali, kwa lengo la kujenga na kudumisha amani, umoja na mshikamano na kamwe dini isiwe ni chanzo cha kinzani na migogoro.

Dr. Bilal anawachangamotisha Wasomi wa Kiislam kutafuta njia na mikakati itakayowawezesha waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo kuheshimiana, kupendana na kuishi pamoja kama ndugu, wakipania kujenga na kuimarisha nchi yao, daima wakitafuta mafao ya wengi.

Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram kinachoendesha mapambano yake nchini Nigeria kimekwisha sababisha mashambulizi kumi na tisa ya kujitoa mhanga kwa kuchoma Makanisa na Misikiti. Nchini Tanzania, Kikundi cha Uamsho kimekuwa kikihusishwa pia na uchomaji wa Makanisa Zanzibar. Hii ni changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali kujikita katika misingi ya imani, maadili na utu wema ili kudumisha amani na utulivu ndani ya Jamii.

Dr. Bilal anawachangamotisha Wasomi wa dini ya Kiislam kuwekeza katika elimu, sayansi na teknolojia, katika masuala ambayo hayatakinzana na imani ya dini yao na sheria maadili katika ujumla wake.







All the contents on this site are copyrighted ©.