2012-12-19 08:09:02

Salam za Noel kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa watoto wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Bambino Gesù


Kardinali Tarcisio Bertone, katibu mkuu wa Vatican, Jumanne tarehe 18 Desemba 2012 alitembelea Hospitali ya Bambino Gesù, inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican ili kuwasalimia watoto wagonjwa waliolazwa Hospitalini hapo pamoja na kuwashirikisha salam na matashi mema ya Siku kuu ya Noeli kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.

Amewapongeza na kuwashukuru wafanyakazi wa Hospitali ya Bambino Gesu kutokana na kuunganisha kwa umakini mkubwa huduma na weledi katika kuwatibu watoto wanaolazwa Hospitalini hapo, hali inayoonesha mshikamano wa dhati miongoni mwa wafanyakazi katika vitengo mbali mbali Hospitalini hapo.

Anasema, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anafuatilia kwa umakini mkubwa huduma mbali mbali zinazotolewa Hospitalini hapo na anawapongeza kwa kufungua tawi jipya la Hospitali ya Bambino Gesù, kwenye eneo la Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya kuta za Roma; kituo ambacho kimepewa jina la Benedikto XVI na kitatumika kwa ajili ya kutoa tiba sanjari na kufanya tafiti.

Kardinali Bertone amefurahi kukutana na watoto wagonjwa wanaotibiwa Hospitalini hapo wakifurahia huduma na tiba, jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele cha pekee kwa kila mtoto. Bado Jumuiya ya Kimataifa imeshikwa na bumbuwazi kutokana na mauaji ya kinyama waliofanyiwa watoto wa mjini Connencticut, nchini Marekani hivi karibuni. Masikitiko kutokana na mauaji ya watoto hao yamegeuka kuwa ni sala kwa kila mtu, lakini hasa wale waliopewa dhamana ya kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia wanatekeleza wajibu wao kikamilifu kwa kulinda maisha ya watoto.

Ili mtoto aweze kukua na kukomaa barabara anahitaji kuonjeshwa furaha na amani, mambo ambayo yanapaswa kuanzia ndani ya familia yenyewe. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anabainisha kwamba, mtoto anahitaji kuonja uwepo wa karibu na matumaini yanayobubujika kutoka katika upendo; haya ndiyo mang'amuzi ya kwanza kabisa ambayo watoto wanapaswa kuyaonja anasema Kardinali Bertone.

Watoto wanapaswa kusaidiwa kupata majibu ya maswali yao ambayo bado yanaelea angani, kwani wana hamu ya kufahamu na kuelewa; utume unaotekelezwa shuleni na ndani ya Familia. Watoto hawa wafahamishwe na kueleweshwa maana ya mateso wanayokabiliana nayo. Huu ni wajibu wa wazazi na walezi kuwasaidia kufahamu undani wa maisha haya ili waweze kujifunza kupenda.

Kardinali Bertone anasema, Siku kuu ya Noeli liwe ni tukio jipya linaonesha utashi na ukarimu wa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya binadamu; anayependa kila kiumbe chake sanjari na kumweka Kristo kuwa ni kiini cha historia ya mwanadamu yaani: Kabla na Baada ya kuzaliwa kwa Kristo; Yeye ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, Nyakati zote ni zake; changamoto ya kuuvua utu wa kale unaogubikwa katika ubinafsi na badala yake kujivika utu mpya na kuanza kutembea katika ukweli na nyakati mpya za uwepo wa Kristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.