Mwaka wa Imani: Wongofu wa ndani, Kanisa na Imani ni maneno yanayopaswa kupewa uzito
unaostahili!
Askofu mkuu Francis Joseph Chaput, wa Jimbo kuu la Philadelphia, Marekani, anabainisha
kwamba, Wongofu wa ndani, Kanisa na Imani ni maneno ambayo yanapaswa kupewa uzito
unaostahili katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.
Ni mwaliko
kwa waamini kuchuchumilia wongofu wa ndani kama sehemu muhimu sana ya utekelezaji
wa utume wake katika ulimwengu mamboleo. Kila mwamini anaalikwa kuwa mtakatifu, wito
na mwaliko kwa kwanza kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Mwamini mwenye Imani thabiti
hawezi kuyumbishwa na kinzani na migogoro inayoletwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia
au kwa watu kupenda kukumbatia mawazo mepesi mepesi hata katika maisha ya ndoa na
familia. Wanandoa wanapaswa kumwongokea Mwenyezi Mungu, daima wakisaidiana katika
hija ya maisha yao ya ndoa, ili kwa pamoja waweze kufikia utakatifu wa maisha. Hizi
ni juhudi zinazohitaji kuimarishana katika imani, mapendo na matumaini.
Askofu
mkuu Chaput anasema kwamba, kuna wakati katika historia ya Kanisa, waamini waliyachukulia
maisha na utume wa Kanisa kama jambo la kawaida na kuyafanya kuwa ni sehemu ya mazoea,
kiasi hata cha kupoteza dhamana na utume wake katika Ulimwengu. Ndivyo inavyoweza
kutokea hata katika maisha ya wanandoa, pale wanapodhani kwamba, maisha yao ni jambo
la kawaida na hakuna jipya, basi hapo wanaweza kuanguka katika utupu na hali ya mazoea.
Kwa
njia ya toba na wongofu wa ndani, Mwenyezi Mungu ameweza kulijalia Kanisa Watakatifu
ambao wamekuwa ni chachu ya wongofu na utakatifu wa maisha kwa mamillioni ya waamini.
Baadhi yao ni: Mtakatifu Bernardo, Mtakatifu Francisco wa Assisi, Theresa wa Avila
na Katarina wa Siena. Ni watakatifu waliolisaidia Kanisa kutubu na kuongoka, likaanza
tena kuchuchumilia hija ya utakatifu katika maisha na utume wake. Ni watu ambao waliwasha
moto wa imani na matumaini mintarafu dhamira ya Kristo mwenyewe.
Hali kama
hii inaendelea kujidhihirisha kwa namna ya pekee kabisa kwa njia ya Vyama vya kitume
ambavyo vimeibuka mara baada ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Ni
vyama ambavyo vinajikita katika kusoma, kutafakari na kumwilisha Injili ya Mapendo.
Vyama hivi ni kielelezo cha neema na huruma ya Mungu kwa Kanisa lake. Kumbe, hakuna
haja ya kuwa na wasi wasi wa uwepo wa Vyama vya Kitume ndani ya Kanisa, bali kila
Chama kitekeleze wajibu na dhamana yake, daima kikijitahidi kudumisha umoja, upendo
na mshikamano na Familia ya Mungu katika eneo husika.
Mama Kanisa daima yuko
katika hija ya toba na wongofu wa ndani, ili aweze kuendelea kuwa ni mwaminifu kwa
Mungu na Kwa Kristo mchumba wake. Ikumbukwe kwamba, Kanisa ni Jumuiya ya Waamini wanaomfuasa
Kristo. Ni Mama na Mwalimu; Kiongozi na Mfariji wa wote wanaoteseka kiroho na kimwili.
Kanisa ni mchumba amini wa Kristo na kwamba ni mali ya Kristo ambaye amewakabidhi
binadamu wenye karama na mapungufu yao kuliongoza. Kanisa linaendelea kufuata msingi
wa Kweli za Kiinjili uliowekwa bayana na Kristo mwenyewe kwa njia ya Neno la Mungu
na Mapokeo hai.
Waamini wanakumbushwa kwamba, hawawezi kamwe kuwa na Mungu
kama Baba yao bila kuwa na Kanisa kama Mama yao, kama alivyosema Mtakatifu Cypriani;
kila mwamini anapaswa kujisikia kuwa ni sehemu ya Kanisa. Kanisa halina budi kuwa
ni sehemu ya maisha na utume wa kila mwamini; mahali ambapo wanashibishwa na Neno
la Mungu, Maisha ya Kisakramenti na Katekesi ya kina.
Kanisa ni uwanja ambapo
waamini kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao wanatangaza kwa ujasiri mkubwa Injili ya
Upendo unaoonesha Imani wanayokiri kwa vinywa vyao, Imani wanayoiadhimisha kwa njia
ya Sakramenti za Kanisa; Imani wanaojitahidi kuimwlisha kwa kufuata Amri za Mungu
ambazo ni dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu.
Utume ni mwanzo na
kilele cha maisha ya Kanisa linaloendelea kutekeleza kwa dhati kabisa ile Amri ya
Kristo, nendeni ulimwenguni kote mkawafanye watu wote kuwa ni wanafunzi wangu. Huu
ni ujumbe ambao unamgusa kila mfuasi wa Kristo tangu wale wa Kanisa la Mwanzo hadi
leo hii katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.
Utume wa Kanisa
unapata chimbuko lake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Waamini kwa pamoja,
wanachangamotishwa na Mama Kanisa kushiriki katika kazi ya Ukombozi iliyoanzishwa
na Kristo mwenyewe yapata miaka elfu mbili ya ukristo, wakitambua kwamba, Yesu mwenyewe
yuko pamoja nao hadi utimilifu wa dahali, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Imani
yao kwa Kristo inaendelea kuwa hai daima.
Askofu mkuu Chaput anakumbusha kwamba,
Imani kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kumbe mwamini ana uhuru kamili
wa kuipokea na kuifanyia kazi au kuikataa na hatimaye, kumezwa na malimwengu. Mwenyezi
Mungu ndiye anayejitaabisha kukutana na mwamini kwa njia ya Yesu Kristo na Kanisa
lake, ndiyo maana waamini wanayo haki ya kuendelea kumtumainia Yesu Kristo Mkombozi
wa dunia. Imani ni jiwe kuu katika maisha ya mwamini, lakini Imani bila matendo hiyo
inakufa na kunyauka.