Bikira Maria ni kielelezo cha Imani na Matumaini thabiti kwa ahadi za Mwenyezi Mungu
aliyemwezesha kuwa ni Mama wa Mungu
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa Katekesi yake katika Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani, Jumatano tarehe 19 Desemba 2012, ameyaelekeza mawazo yake katika
kipindi hiki cha Majilio, kwa kutafakari Imani ya Bikira Maria, Mama wa Kristo.
Malaika
Gabrieli aliyetumwa na Mungu kwenda kumpasha habari Bikira Maria kuwa atakuwa Mama
wa Mungu, alianza kwa mwaliko kwa Bikira Maria kufurahi kwani Bwana alikuwa pamoja
naye. Hii ndiyo furaha ya matumaini ya Kimasiha inayowabubujikia watu wa Mungu na
kwa namna ya pekee Binti Sayuni ambaye amejaa neema.
Ni matunda ya neema yanayoujaza
Moyo wa Bikira Maria kiasi cha kujaza ile fadhila ya utii kwa Neno la Mungu. Imani
ya Bikira Maria kama ilivyokuwa Imani ya Abraham, inafumbata kwa namna ya ajabu imani
kwa ahadi za Mungu hata bila kufahamu undani wake. Katika maisha yake, Bikira Maria
alifahamu, kama wanavyofahamu waamini wengine kwamba, utashi wa Mungu wakati mwingine
unafifia kiasi hata cha kutoweka katika matarajio ya waamini; hali hii anasema Baba
Mtakatifu inakumbatia Fumbo la Msalaba.
Ni jambo la muhimu sana kwamba, Bikira
Maria anapopashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu, anafikiri mno moyoni mwake
maana ya ujumbe kutoka kwa Malaika Gabrieli. Kwa mfano wa Bikira Maria, waamini wanakumbushwa
kuwa imani, licha ya kuwa ni utii kwa utashi wa Mungu, lakini haina budi kuimarisha
katika uelewa na kupokea mapenzi ya Mungu kila siku.
Kipindi hiki kitakatifu
kinachowaelekeza waamini katika Maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho, Sala ya Bikira
Maria iwasaidie waamini kuwa wanyenyekevu, wanaoamini katika imani inayowafungulia
malango ya neema ya Mungu katika mioyo na ulimwengu kwa ujumla. Waamini wajifunze
fadhila ya unyenyekevu katika kutekeleza mapenzi ya Mungu kama alivyofanya Bikira
Maria hata akawezeshwa kuwa ni Mama wa Mkombozi; Neno wa Mungu akafanyika mwili.
Bikira
Maria ni kielelezo makini cha utii na msikivu wa Neno la Mungu, awawezeshe waamini
kujiandaa kikamilifu kumpokea Mkombozi anayekuja kati yao!