Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Asia, katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, linalenga
kuwasaidia waamini kumwilisha Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake katika medani mbali
mbali za maisha; wakitambua kwamba, wanakabiliana na changamoto ya kumwilisha Imani
hii kwa njia ya majadiliano ya kidini na kiekumene; daima wakiwa wameshikamana katika
kutafuta ukweli.
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani Barani Asia, yanakwenda sanjari
na changamoto mbali mbali zilizoibuliwa wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu
juu ya Uinjilishaji Mpya sanjari na Jubilee ya miaka hamsini ya Mtaguso Mkuu wa Pili
wa Vatican. Bara la Asia ni kubwa na kila nchi ina vipaumbele vyake; lakini kwa pamoja
wanaunganishwa na dhamana ya kuendeleza majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya
Kiislam, ambao katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na kinzani kubwa
pamoja na madhulumu ya kidini.
Dhamana ya pili ni kujenga utamaduni wa kutafuta
haki, amani na upatanisho wa kweli kwa kutambua tofauti za kidini, kiimani na kitamaduni
zinazojitokeza kati yao na kwamba, huu ni utajiri mkubwa unaoweza kutumiwa kujenga
na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa, kwa kutafuta mafao ya wengi.
Maaskofu
Katoliki Barani Asia, wanatambua na kuthamini maendeleo makubwa yanayojionesha katika
sekta ya sayansi na ukuaji wa uchumi. Wanasema ni wajibu wao kusaidia Jamii kuhakikisha
kwamba, maendeleo haya yanakumbatia pia misingi ya maadili na utu wema, Mwenyezi Mungu
akipewa pia kipaumbele cha kwanza, vinginevyo, watu wengi watajikuta wanatumbukizwa
katika ombwe na utupu! Matokeo yake ni kudhalilisha utu na heshima ya binadamu pamoja
na kuongezeka kwa baa la umaskini.
Maendeleo ya kiuchumi, yajengeke katika
misingi ya: ukweli, uwazi, uaminifu pamoja na uwajibikaji fungamanishi; daima wanasiasa
na watunga sera wakijitahidi kutafuta mafao ya wengi kwa kutoa huduma makini na endelevu
inayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Vijana wajengewe misingi
bora ya elimu, itakayowawezesha kupambana vyema na mazingira, ili kuzifanya nchi zao
kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Maendeleo ya sayansi na teknolojia, kimsingi
hayakinzani na imani, bali yanategemeana. Ni matumaini ya Maaskofu wa Asia kwamba,
waamini wataweza kutolea ushuhuda wa imani yao kwa njia ya maisha adili na aminifu
yanayojikita katika Kweli za Kiinjili.