Yaliyojiri katika maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 100 ya Imani Katoliki Kaskazini
mwa Uganda
Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu
yuko nchini Uganda kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilee ya Miaka mia moja ya Imani
Katoliki Jimbo la Arua na katika Jimbo kuu la Gulu. Aliwasili nchini Uganda tarehe
13 Desemba 2013, akaongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa waamini wa Jimbo kuu la Gulu.
Akapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Kamati ya Ukarabati Kanisa kuu la Arua.
Alizindua maadhimisho ya Jubilee ya miaka 100 kwa mashindano ya mpira wa miguu. Alipata
nafasi ya kusali masifu ya jioni na Watawa wanaoishi katika Monasteri ya Utatu Mtakatifu.
Tarehe
14 Desemba 2013, Kardinali Filoni na ujumbe wake walifanya hija kwenye Kanisa la Lodonga,
akaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na Mapadre pamoja na Watawa wanaoishi na kutekeleza
utume wao kwenye Jimbo kuu la Gulu, Uganda. Alipata nafasi ya kutembelea Parokia ya
Moyo.
Jumamosi tarehe 15 Desemba 2013 aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu
kwa Waseminari wanaotoka Jimbo kuu la Gulu. Akawakumbusha umuhimu wa kudumisha umoja
na mshikamano; dhamana ya Seminari; umuhimu wa kuzingatia muda wa malezi wawapo Seminarini
kama kipindi cha kung’amua wito wao, kujifunza na kuboresha maisha yao ya sala na
kiroho.
Ni muda wa masomo na fursa makini ya kujenga na kudumisha uhusiano
na Yesu Kristo kwa njia ya Ibada kwa Ekaristi Takatifu; kwa kuwa waaminifu kwa Kristo
na Kanisa lake sanjari na kuzingatia mafundisho, wakiwa tayari kuyatolea ushuhuda
makini. Anawataka Majandokasisi kuwa shujaa na imara katika imani, wakikumbatia ndani
mwao maisha ya useja tayari kuendeleza urithi wa Mama Kanisa kutoka kwa Mababa wa
Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ili Kuinjilisha kwa ari, kasi na moyo mkuu zaidi.
Jioni,
Kardinali Filoni alibahatika kuzungumza na baadhi ya Maaskofu Katoliki Uganda, kadiri
ya shida zao na baadaye alikutana na Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda na kuwataka
kuendeleza ule moyo, kasi na ari ya kimissionari kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao,
kama walivyofanya Mashahidi wa Uganda wanaoheshimiwa na Mama Kanisa.
Wawasaidie
waamini kutambua thamani ya utu wao kwa njia ya Injili, ili wote kwa pamoja waweze
kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa. Maaskofu wajikite zaidi katika kujenga
na kuimarisha umoja, haki, amani na upatanisho ili kuondokana na chuki, uhasama na
vita ambayo imesababisha mateso na magumu mengi kwa wananchi wa Uganda.
Anawahimiza
kukuza na kuimarisha imani, hasa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Washirikiane
kwa karibu zaidi na Mapadri wao katika utekelezaji wa majukumu ya kufundisha, kuongoza
na kuwatakatifuza watu wa Mungu nchini Uganda.
Wawasaidie Watawa kumwilisha
karama za mashirika yao katika maisha na utume wa Kanisa mahalia. Wakazie majiundo
endelevu kuhusu: Katekesi, Liturujia, Matendo ya huruma kama njia ya kumwilisha Neno
la Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu, bila kusahau kuhusu Mafundisho Jamii ya
Kanisa, kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu.
Familia iwe ni Kanisa dogo
la nyumbani, wazazi waoneshe mifano bora na utakatifu wa maisha; daima wakiwa waaminifu
sanjari na kuthamini utu wa kila mtu. Maaskofu wawe wasimamizi waaminifu wa mali ya
Kanisa katika Majimbo yao. Wajichotee utajiri wa Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili
wa Vatican, Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki na Mafundisho Jamii ya Kanisa.
Jumapili
tarehe 16 Desemba 2012 Kardinali Filoni na ujumbe wake walifanya hija ya kiroho kwenye
madhabau ya Indriani pamoja na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Tarehe 17 Desemba
2012, Kardinali Fernando Filoni na Ujumbe wake, wameondoka kutoka Gulu kurudi Vatican
ili kuendelea na majukumu mengine ya kitume. Haya ndiyo yaliyojiri katika maadhimisho
ya Jubilee ya Miaka 100 ya Ukristo Jimbo Katoliki Arua, Uganda.