2012-12-17 09:46:16

Wongofu wa ndani unajikita katika haki, ukweli na upendo!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 16 Desemba 2012, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alitafakari juu ya mwaliko na changamoto iliyotolewa na Yohane Mbatizaji wakati alipokuwa anahubiri kuhusu Ubatizo wa toba na maondoleo ya dhambi, kwenye Ukingo wa Mto Yordani. Majadiliano kati ya watu mbali mbali waliofika kubatizwa na Yohane Mbatizaji yana umuhimu wa pekee hata katika Jamii ya leo.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, mkazo wa pekee unaotolewa na Yohane Mbatizaji katika mahubiri yake ni kuzingatia kanuni ya haki inayomwilishwa katika mapendo; kuweka uwiano na matumizi bora ya mali kwa kuonesha mshikamano na watu wanaohitaji badala ya mtu kujifungia katika ubinafsi wake, kwani haki na upendo ni fadhila zinazokumbatiana. Upendo unahitajika hata katika Jamii ambamo haki inapewa kipaumbele cha kwanza, kwani daima katika maisha kuna watu wanaohitaji msaada wa hali na mali.

Baba Mtakatifu anasema, Yohane Mbatizaji aliwaambia watoza ushuru waendelee kutekeleza wajibu wao vyema na wala wasitake kubadili, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, hawatumii fursa hizi kwa ajili ya kuiba, bali watekeleze wajibu na dhamana waliyokabidhiwa na Jamii kwa ukweli, uwazi na uaminifu. Hatua ya kwanza katika kuelekea maisha ya uzima wa milele ni kutekeleza Amri za Mungu, na kwa nafasi hii, watoza ushuru wanaambiwa wasiibe!

Baba Mtakatifu anasema, Askari ni watu ambao wamepewa madaraka makubwa na Jamii, wakati mwingine wanashawishika kuyatumia vibaya maadaraka haya. Jibu la Yohane Mbatizaji ni kwamba, Askari kamwe wasiwadhulumu wala kuwabambikia watu mashitaka ya uongo na waridhike na mishahara yao! Hapa inaonesha kwamba, wongofu wa ndani unaanza katika uaminifu na heshima kwa wengine. Hii ni kanuni maadili inayomgusa kila mtu, lakini zaidi kwa wale waliyopewa dhamana na Jamii husika.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Mwenyezi Mungu atamhukumu kila mtu kadiri ya matendo yake, changamoto ya kufuata na kutekeleza Mapenzi ya Mungu. Kwa hakika dunia ingeweza kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi ikiwa kama kila mtu angeweza kutekeleza kanuni maadili zilizotolewa na Yohane Mbatizaji. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kusali na kumwomba Bikira Maria ili aweze kuwasaidia katika maandalizi ya Maadhimisho ya Noeli, kwa kuzaa matunda ya wongofu wa ndani.

Mara baada ya Tafakari ya Sala ya Mchana, Baba Mtakatifu alirudia tena ombi lake kwa Familia na Parokia zilizoko mjini Roma, kuonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa Vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taize, watakaokusanyika mjini Roma kuanzia tarehe 28 Desemba 2012 hadi tarehe 2 Januari 2013 kwa ajili ya kusali. Anawashukuru wote ambao wameonesha nia ya kuwapokea na kuwasetiri vijana hawa kwenye Familia na Parokia zao, kama kielelezo makini na mshikamano kwa vijana hawa wanaopenda kufanya mang'amuzi ya upendo wa kikristo.

Baba Mtakatifu amesikitishwa sana na mauaji ya watu ishirini na wanane, kati yao kuna watoto ishirini, yaliyotokea huko Newtown, Connecticut, nchini Marekani. Anawahakikishia wote walioguswa na msiba huu kwamba, yuko pamoja nao kwa njia ya sala na anawaombea faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kipindi cha Majilio iwe ni fursa ya kusali na kujikita zaidi katika kudumisha amani.

Baba Mtakatifu pia alitumia fursa hii kwa ajili ya kubariki sanamu za Mtoto Yesu zilizokuwa zimeletwa na watoto kutoka katika Parokia mbali mbali za Jimbo kuu la Roma kwa ajili ya kubarikiwa na hatimaye, kuziweka kwenye Mapango ya Noeli.







All the contents on this site are copyrighted ©.