2012-12-17 14:24:42

Rais Mahmoud Abbas wa Palestina akutana na kuzungumza na Papa Benedikto XVI mjini Vatican


Baba Mtakatifu Benedikto wa Kumi na sita, Jumatatu, tarehe 17 Desemba 2012 amekutana na kuzungumza na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas ambaye amekutana pia na viongozi waandamizi kutoka Vatican chini ya Kardinali Tarcisio Bertone, katibu Mkuu wa Vatican.

Viongozi hawa wawili wamezungumzia pamoja na mambo mengine kuhusu Azimio la Umoja wa Mataifa lililotoa fursa kwa Palestina kuwa ni nchi mwanachama mtazamaji wa Umoja wa Mataifa. Ni matumaini ya viongozi hawa wawili kwamba, juhudi hizi za Jumuiya ya Kimataifa, hatimaye, utaupatia mgogoro kati ya Palestina na Israeli suluhu ya kudumu, kwa kuheshimiana na kudumisha haki kwa pande zote mbili.

Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake, wamejadili pia hali ya migogoro na kinzani zinazojitokeza huko Mashariki ya Kati, wakiwa na tumaini kwamba, hatimaye, wahusika wataweza kuanzisha mchakato wa upatanisho wa kitaifa, ili amani iweze kutawala. Viongozi hao wamejadili jinsi ambavyo Jumuiya ya Kikristo inavyoweza kuchangia katika maendeleo, ustawi na mafao ya wengi nchini Palestina na huko Mashariki ya Kati.







All the contents on this site are copyrighted ©.