Parokia iwe ni mahali pa kusikiliza na kutafakari Neno la Mungu; Maadhimisho ya Sakramenti
za Kanisa na Majiundo endelevu katika Imani
Kipindi cha Majilio ni wakati muafaka kwa waamini kutubu na kuongoka, tayari kumpokea
Mwana wa Mungu anayezaliwa kati yao. Kanisa linamngoja Mkombozi wa dunia kwa moyo
wa furaha; mwaliko wa pekee katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya tatu ya
Kipindi cha Majilio.
Hii ndiyo furaha iliyooneshwa kwa namna ya pekee na Bikira
Maria alipopashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu.Hakuna sababu ya kuhuzunika
wala kukata tamaa kwani uwepo wa Yesu Kristo Mkombozi wa Ulimwengu unaleta vijito
vya furaha katika maisha ya waamini.
Ni maneno ya Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita, wakati wa mahubiri yake aliyoyatoa kwenye Parokia ya Mtakatifu Patrizio,
iliyoko nje kidogo ya Mji wa Roma, wakati wa ziara yake ya kichungaji, Jumapili iliyopita,
tarehe 16 Desemba 2012. Waamini wanapaswa kutambua kwamba, kweli Mungu yuko pamoja
nao na wala hayuko mbali; anajionesha katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu
na katika Uhai wa Kanisa. Mwaliko ni kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anakuwa
ni mjumbe wa uwepo endelevu wa Mungu katika ulimwengu na kwa njia hii, wataweza kupata
furaha inayobubujika kutoka kwa Mungu mwenyewe!
Baba Mtakatifu anasema, hakuna
jambo lolote linaloweza kuwatenganisha waamini na upendo wa Kristo, ikiwa kama watajitenga
na dhambi na daima wawe wapesi kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika Sakramenti
ya Upatanisho. Anawaalika waamini kusali kwa bidii kwani Mungu anawasikiliza, anawafahamu
na anawatekelezea maombi yao, hata kama si kama vile walivyoomba. Furaha inayobubujika
kutoka kwa Mwenyezi Mungu ikutane na upendo wa binadamu unaopania kutekeleza mapenzi
yake kwa moyo wa ukarimu na kamwe ubinafsi usipate nafasi.
Yohane Mbatizaji
aliyetambua dhamana na utume wake wa kumwandalia Yesu Njia, anawaonesha wafuasi wa
Kristo namna ya kumfuasa kwa ujasiri na uaminifu mkuu wakiwa tayari kubadili maisha
yao, ili kukutana na Kristo anayebatiza kwa Maji na Roho Mtakatifu ili kusafisha maisha
ya watu wake na hatimaye, kujenga umoja na kuendelea kufurahia amani na utulivu hata
nyakati za magumu na udhaifu wa kibinadamu.
Baba Mtakatifu amewashukuru na
kuwapongeza wadau mbali mbali wanaojitoa kimasomaso kwa ajili ya Uinjilishaji mpya
Parokiani hapo. Anawapongeza watoto ambao wanajiandaa kwa ajili ya kupokea Sakramenti
ya Ekaristi Takatifu pamoja na kuimarishwa kwa Kipaimara, kielelezo makini cha uhai
wa Kanisa. Parokia hii iliyozinduliwa kunako mwaka 2007 iwe ni mahali pa kusikiliza
Neno la Mungu, kuadhimisha Sakramenti za Kanisa na kujichotea nguvu na neema katika
hija ya maisha, daima wajikitahidi kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano
wa dhati.
Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kiwe ni kiini cha maisha
ya mwamini binafsi na Jumuiya; changamoto ya kuendelea kutambua umuhimu wa Jumapili
kuwa ni Siku ya Mungu, Siku ya Kristo, Siku ya Kanisa na Siku ya Mwanadamu; inayowapatia
fursa ya kuadhimisha Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo. Waamini waonje huruma
na upendo wa Mungu kwa njia ya sakramenti ya Upatanisho.
Baba Mtakatifu anasema,
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, iwe ni fursa ya kujikita katika Katekesi ya kina, kwa
kujifunza Kanuni ya Imani, kama njia ya kukutana na Mungu aliye hai katika hija ya
maisha yao ya kila siku. Ni mwaliko kwa Familia kutekeleza wajibu wake kwa upendo,
ukarimu na uwepo wao. Vijana wajifunze kuwa wasikivu kwa walezi wao wakitambua kwamba,
wao pia ni wadau katika Uinjilishaji Mpya.