2012-12-17 09:14:18

Kampeni ya Usaid Gimbuka yazinduliwa rasmi nchini Rwanda ili kupambana na hali ngumu ya maisha


Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Rwanda, Caritas Rwanda, hivi karibuni kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Marekani, USAID limezindua kampeni ya miaka mitatu kuanzia mwaka 2013 – 2015 ijulikanayo kama “Usaid Gimbuka”, inayolenga kuziwezesha familia zinazokabiliana na hali ngumu ya maisha kuanzisha miradi ya kujitegemea. Mradi huu utatekelezwa kwenye wilaya kumi na nne nchini Rwanda.

Akizindua mradi huu Mheshimiwa Padre Oreste Incimata, Katibu mkuu wa Caritas Rwanda anasema, huu ni mradi ambao umekuwa ukitekelezwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda tangu mwaka 1960. Juhudi za Kanisa zimekuwa zikielekezwa zaidi kwenye huduma ya afya, huduma za kijamii pamoja na huduma za maendeleo endelevu kwa kuwafaidisha waamini katika Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo.

Caritas Rwanda imeendelea kuku ana kupanuka, hadi sasa imefikia kiwango cha kujitegemea katika shughuli zake za utoaji huduma na maendeleo kwa Jamii ya watu wa Rwanda na kwamba kwa sasa inapokea kiwango kidogo sana cha misaada kutoka nje. Ukomavu huu ni matunda ya ushirikiano kati ya Caritas Rwanda na Usaid. Mradi huu katika kipindi cha miaka mitatu unapania pamoja na mambo mengine kuboresha afya na lishe ya wanawake wajawazito; wanawake walioathirika kwa Virusi vya Ukimwi.

Walengwa wengine ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano bila kuwasahau watoto yatima kwa kuwajengea uwezo wa kwenda shule, ili kupata elimu itakayowawezesha kukabiliana na maisha yao kwa sasa kwa siku za usoni. Caritas Rwanda inapenda pia kuwawezesha wakulima wadogo wadogo kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu ili kupambana na baa la umaskini kwa kuwahifadhia pia mazao ya kilimo. Kuna mtindo kwa baadhi ya wafanyabiashara kupandisha na kupunguza bei ya mazao ya wakulima, hali ambayo wakati mwingine inaleta hasara kubwa kwa wakulima, wakati ambapo wafanyabiashara wanaendelea kufaidika zaidi.

Kwa upande wake, Bwana Silver Richard, mwakilishi wa Usaid nchini Rwanda anasema, mradi huu unapania kupunguza kwa asilimia walau arobaini na nne ya watoto wanaodumaa kutokana na kushambuliwa na utapiamlo w akutisha nchini Rwanda.








All the contents on this site are copyrighted ©.