Uinjilishaji Mpya unajikita katika: Katekesi ya kina, maisha adili, ukweli na uwazi!
Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika
na Magascar, SECAM katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha umuhimu wa
viongozi wa Kanisa Barani Afrika kutoa katekesi ya kina inayopata chimbuko lake katika
mafundisho tanzu ya Kanisa, maisha adili, ukweli, uwazi kama sehemu ya mchakato wa
Uinjilishaji Mpya, dhamana inayotekelezwa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia
ya tatu ya Ukristo.
Vyama vya
kitume ndani ya Kanisa havina budi kupewa katekesi ya kina inayogusa kwa undani zaidi
kuhusu: Imani, Sakramenti, Maisha adili na Sala, ili wanachama wa vyama hivi waweze
kufahamu lengo pamoja na kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, daima
wakipania kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao kuyatakatifuza malimwengu; vinginevyo,
wanaweza kujikuta wamepotoka.
Kardinali Pengo anawahimiza Viongozi wa Kanisa
kuwa karibu na tayari kutoa katekesi ya kina inayojengeka katika mhimili wa maisha
adili na nyofu; ukweli na uwazi, kwani hii ni changamoto kubwa kwa Mama kanisa wakati
huu linahamasisha juhudi za Uinjilishaji Mpya. Toba na wongofu wa ndani pamoja na
ushuhuda wa Imani katika matendo ni mambo msingi kwa wakati huu.