2012-12-15 12:15:14

Jengeni utamaduni wa kuheshimiana na kuthaminiana kama njia ya upatanisho, haki na amani nchini Kenya!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linaendelea kujizatiti ili kuhakikisha kwamba, uchaguzi mkuu nchini humo unaotarajiwa kufanyika tarehe 4 Machi 2013 unatawaliwa na misingi ya haki na amani. Ni matumaini ya Maaskofu wa Kenya kwamba, matatizo yaliyojitokeza kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 - 2008 hayatajirudia tena. Kanisa Katoliki litaendelea kusimamia mafao ya wengi na wala haliwezi kupendelea upande wowote kama ambavyo baadhi ya wanasiasa walilishutumu kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Hayo yamebainishwa na Mheshimiwa Padre Vincenti Wambugu, katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, alipokuwa anazungumza na viongozi wandamizi wa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Kenya, CRS hivi karibuni. Anasema, kuna vitendo vya uvunjifu wa misingi ya amani na utulivu vinavyoendelea sehemu mbali mbali za Kenya kama vile mauaji yaliyotokea kwenye Bonde la Mto Tana pamoja na vitendo vya kigaidi huko Garisa. Hii ni hali tete inapaswa kushughulikiwa kikamilifu kwa kuzingatia sheria za nchi.

Inasikitisha kuona kwamba, hata baada ya kupitisha Katiba Mpya ya Kenya, bado Wananchi wengi wa Kenya wamegawanyika katika misingi ya ukabila na mahali anapotoka mtu, badala ya kujenga na kudumisha misingi ya upendo, amani na mshikamano wa kitaifa. Ni jukumu la viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajenga na kuimarisha mshikamano wa kitaifa, kwa kuzingatia misingi ya haki na amani.

Ndiyo maana Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika Kampeni ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2012 walikazia umoja na amani, kama njia ya kuonesha mabadiliko ya kweli.

Padre Wambugu anakazia umuhimu wa kukuza na kudumisha utamaduni wa kuheshimiana na kuthaminiana kama watu binafsi, makundi na watu wote. Hii ni hatua kubwa katika mchakato wa kujenga misingi ya haki, amani na upatanisho wa kweli. Watu wakubali na kuthamini tofauti walizonazo kama sehemu ya utajiri wao na wala si kikwazo cha mshikamano na umoja wa kitaifa. Kutokubali, kutambua na kuthamini tofauti hizi, kunaweza kupelekea uvunjifu wa misingi ya haki, amani na utulivu nchini Kenya kama ilivyojitokeza kwa nafasi mbali mbali nyakati za uchaguzi mkuu.







All the contents on this site are copyrighted ©.