2012-12-15 13:29:22

Dumisheni amani Ghana, msiwatumbukize wananchi katika maafa baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana linavisihi vyama vya kisiasa nchini humo vilivyoshiriki katika uchaguzi mkuu uliohitimishwa hivi karibuni, kuhakikisha kwamba, wanajikita katika kutafuta mafao ya wengi, wakijitahidi kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu.

Ujumbe huu unafuatilia cheche za vurugu na kinzani zinazoanza kujitokeza nchini humo ili kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu ambamo Rais John Mahama wa Chama cha NDC ameibuka kidedea kwa kuwabwaga wapinzani wake. Itakumbukwa kwamba, Rais John Mahama alichukua dhamana hii mara baada ya kifo cha Rais John Atta Mills, kilichotokea mwezi Julai 2012. Wasimamizi wa uchaguzi ndani na nje ya Ghana, katika taarifa yao wanasema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki, lakini tamko hili linapingwa vikali na Nana Akufo Addo kutoka Chama cha Upinzani.

Maaskofu wanawataka wananchi wa Ghana kulinda na kudumisha amani ambayo kwa miaka mingi imekuwa ni urithi wao wanaojivunia kwa kipindi cha miaka mingi, wakiipoteza watajutia na itawagharimu sana kuipata tena. Wananchi wa Ghana wanapaswa kujifunza somo kutoka katika nchi ambazo hadi leo hii baada ya uchaguzi zimeendelea kulumbana na kusigana: Kenya, Zimbabwe, Pwani ya Pembe na Nigeria. Chama cha Upinzani kinapania kuwasilisha ombi lake la kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu mahakama kuu.

Ghana kwa miaka mingi imekuwa ikihesabiwa kuwa ni kati ya mataifa machache Barani Afrika ambayo yameendelea kufurahia amani na utulivu; kwa kurithishana madaraka kwa njia ya demokrasia tangu mwaka 1981. Watu wamekuwa wakiheshimu utawala wa sheria na demokrasia.







All the contents on this site are copyrighted ©.