Kuna mamillioni ya watu duniani yanalazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na: vita,
maafa asilia, kinzani na migogoro isiyokuwa na majibu!
Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za
Umoja wa Mataifa zilizoko Geneva, hivi karibuni, wakati akichangia hoja kwenye kikao
cha mia moja na moja cha Baraza la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wahamiaji alisema
kwamba, kuna jumla ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum zaidi ya millioni
sabini na mbili, ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita, maafa
asilia, miradi ya maendeleo na kinzani za kisiasa ambazo Jumuiya ya Kimataifa imeshindwa
kuzidhibiti.
Wimbi la wahamiaji na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za
dunia, linahitaji jibu makini kutoka kwa Jumuiya ya Kimataifa inayopaswa kuratibu,
kuonesha ukarimu pamoja na kuwa na sera zinazotekelezeka. Hizi ni kinzani zinazosababishwa
na watu mbali mbali na wakati mwingine, zinachangiwa na Serikali ambazo hazina utawala
bora. Madhara ya kinzani hizi yanajionesha kwa namna ya pekee mijini, hali ambayo
inahitaji kudumisha utawala wa sheria unaozingatia pia haki msingi za binadamu.
Ni
wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kuonesha mshikamano kwani wahamiaji hawa wameachiwa
peke yao kushughulikia hatima ya maisha yao. Kuna watu zaidi ya millioni saba na watu
wasiokuwa na makazi maalum wapatao millioni kumi na tatu ambao kwa miaka kadhaa wamekuwa
wakitafuta kupewa hifadhi kama wakimbizi, lakini juhudi hizi zimegonga mwamba.
Hii
ni rasilimali watu ambayo ingeweza kutumika katika uzalishaji mali kwenye nchi wahisani
badala ya kuonekana kana kwamba, ni kizingiti cha maendeleo, kutokana na sera tenge
na kandamizi dhidi ya wahamiaji na wageni. Hapa kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa
kuingilia kati.
Askofu mkuu Tomasi anaunga mkono wazo la kuanzisha Mfuko wa
Hifadhi ya Dharura kwa Wakimbizi, utakaotumika kujibu kwa haraka zaidi matatizo na
changamoto zinazotokana na wimbi la wahamiaji na wakimbizi, mara zinapojitokeza. Kuna
haja ya kuwa na mikakati madhubuti ya kukabiliana na tatizo la wahamiaji na wakimbizi
kwa kuangalia chanzo kikuu kinachopelekea watu kama hawa kuyakimbia makazi na nchi
zao.
Wachunguzi wa masuala ya kijamii wanabainisha kwamba, umaskini na athari
za myumbo wa uchumi kimataifa ni kati ya mambo makuu yanayopelekea watu wengi kuhama
katika nchi zao wakitafuta fursa za kuboresha hali ya maisha yao. Mambo haya yasipoangaliwa
kwa umakini mkubwa, wahamiaji wanaweza kujikuta wanatumbukizwa katika biashara haramu
ya binadamu, au wanapoteza maisha yao wakiwa njiani kutafuta malisho ya kijani kibichi.
Ikumbukwe
kwamba, wahamiaji wameendelea kuchangia ustawi na maendeleo ya nchi zao licha ya matatizo
na hali ngumu ya maisha wanayokabiliana nayo ugenini. Wamejijengea uwezo wa kujiamini
katika harakati za kuboresha hali yao ya maisha kwa kufanya kazi bila kuchagua. Ni
watu wanaochangia pia ustawi na maendeleo ya nchi wahisani. Tatizo kubwa linalojitokeza
ni ukosefu wa sera makini katika kuwashirikisha wahamiaji katika shughuli za uzalishaji
na maendeleo.
Ujumbe wa Vatican kwenye mkutano huu unabainisha kwamba, wahamiaji
kimsingi ni rasilimali watu kwa ajili ya maendeleo ya Jamii; wanachangia katika maendeleo
na kamwe si kizingiti cha ustawi wa nchi wahisani. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuhakikisha
kwamba, haki msingi za wahamiaji na wakimbizi zinalindwa na kuheshimiwa.