Ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa Siku ya Vijana Duniani 2013
Nendeni ulimwenguni kote mkayafanye mataifa yote kuwa ni wanafunzi wangu ndiyo kauli
mbiu inayoongoza maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani itakayoadhimishwa Rio
de Janeiro, Brazil, mwezi Julai 2013.
Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, anachukua fursa hii kuwaalika vijana kutoka sehemu mbali
mbali za dunia kushiriki katika tukio hili muhimu katika maisha ya imani. Sanamu ya
Kristo Mfalme inayopendezesha mji wa Rio de Janeiro, Brazil, ikiwa na mikono wazi,
ni kielelezo cha mwaliko wa Kristo ambaye yuko tayari kuwapokea wote wanaomwendea
na kwamba, moyo wake unaonesha upendo wa hali ya juu kabisa kwa kila kijana.
Huu
ni mwaliko kwa vijana wenyewe kujiachilia mikononi mwa Kristo. Baba Mtakatifu anawaalika
vijana kushirikisha mang’amuzi haya kwa vijana wenzao watakaoshiriki katika maadhimisho
ya siku ya vijana duniani kwa mwaka 2013 nchini Brazil. Vijana wanapaswa kupokea na
kuukumbatia upendo wa Kristo, ili waweze kuwa ni mashahidi wa upendo huu ambao unatakiwa
kwa kiasi kikubwa ulimwenguni.
Baba Mtakatifu anasema kwamba, vijana wengi
kutokana na kipaji chao cha kujitolea wamesaidia kwa namna ya pekee katika ujenzi
wa Ufalme wa Mungu na maendeleo ya ulimwengu huu kwa njia ya kutangaza Habari Njemaya
Wokovu. Ni watu wenye ari inayopata chimbuko lake kutoka katika Injili ya upendo wa
Mungu unaojionesha kwa njia ya Kristo; walitumia nyenzo na vifaa mbali mbali vilivyokuwepo
kwa wakati ule, pengine duni kuliko hali ilivyo kwa sasa.
Vijana wanaendelea
kujiuliza umuhimu na maana ya maisha pamoja na hali ngumu wanayokabiliana nayo. Matatizo
na changamoto wanazokumbana nazo katika hija ya maisha, vijana wanajiuliza ikiwa kweli
wanaweza kufanya jambo lolote?
Mwanga wa Imani anasema Baba Mtakatifu unaondoa
giza hili kwa kutambua kwamba, maisha ya binadamu ni jambo nyeti sana kwani ni matunda
ya upendo wa Mungu. Mungu anawapenda wote hata wale ambao wamekengeuka na kupoteza
imani yao. Mwenyezi mungu anaendelea kuwasubiri kwa utulivu. Ndiyo maana alimtoa Mwanaye
wa pekee ili aweze kufa na kufufuka kutoka katika wafu ili kumkomboa mwanadamu kutoka
katika utumwa wa dhambi.
Mama Kanisa anapoendelea kutekeleza dhamana na utume
wake wa Uinjilishaji anawategemea vijana, kwani wao ni Wamissionari wa kwanza kabisa
miongoni mwa vijana wenzao. Mara baada ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican,
Papa Paulo wa sita, alitoa ujumbe kwa vijana ulimwenguni, akiwataka kujenga dunia
bora zaidi, kuliko ilivyokuwa kwa wakati ule. Mwaliko huu bado ni endelevu hata leo
hii, licha ya muda kuendelea kuyoyoma kwa kasi. Maendeleo ya sayansi na teknolojia
yanawezesha mwingiliano wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Utandawazi
wa mwingiliano huu unaweza kuwa na mwelekeo chanya katika kukuza ubinadamu, ikiwa
kama utasimikwa katika upendo wa dhati na badala ya kujikita katika vitu! Ni upendo
tu, unaoweza kusheheni katika mioyo ya watu, kwa sababu Mungu ni upendo. Mwanadamu
anapomsahau Mwenyezi Mungu, anapoteza tumaini na upendo kwa wengine. Ndiyo maana kuna
haja ya kumshuhudia Mungu ili watu wengine waweze kuonja uwepo wake. Wokovu wa watu
wote na kila mmoja unategemea kwa kiasi kikubwa upendo huu.
Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya VIjana Duniani
anawakumbusha kwamba, wito wa kimissionari ni muhimu sana kwa ajili ya hija ya imani,
wanapotangaza Injili pamoja na kuwawezesha wao wenyewe kukua na kukomaa kikristo wakishikamana
na Kristo. Hawataweza kuwa waamini ikiwa kama hawawezi kuinjilisha. Kuwa mmissionari
maana yake ni kuwa kwanza kabisa mfuasi wa Kristo, kwa kumsikiliza kwa makini na hatimaye,
kumfuasa.
Baba Mtakatifu anawaalika vijana kufanya tafakari ya kina kuhusu
karama walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu ili waweze kuzitumia kwa ajili ya jirani zao;
wajifunze kusoma historia ya maisha ya kila mmoja wao na kuchuchumilia utajiri urithi
mkubwa waliobahatika kuupata kutoka kwa vizazi vilivyopita, kwa kutambua kwamba, wanaunganishwa
na umati mkubwa wa watu waliotangaza na kurithisha imani ambayo wanapaswa kuwamegea
wengine. Kama Wamissionari wanapaswa kutambua Mapokeo ya Imani ya Kanisa. Vijana wanapaswa
kutambua kile wanacho amini ili kuweza kukitangaza.
Yesu aliwatumwa mitume
wake kwenda ulimwenguni kote ili kutangaza Habari Njema kwa kila kiumbe, yule atakayeamini
na kubatizwa atapata uzima wa milele. Kuinjilisha maana yake ni kutangaza Habari Njema
ya Wokobu ambayo ni Yesu Kristo mwenyewe. Kadiri watakavyomfahamu Kristo ndivyo watakavyokuwa
na hamu ya kutaka kumtangaza zaidi na zaidi; kwa kumpenda na kuvutwa kwake ili kuwa
naye karibu zaidi, kwani ana nguvu ya upendo inayoongoza utume wa kutangaza Injili.
Roho wa Bwana anawataka kujitoa katika ubinafsi wao na kuwa tayari kwenda Kuinjilisha,
daima wakijikita katika nguvu ya upendo wa Mungu, inayowabandua kutoka katika ubinafsi,
ulimwengu, matatizo na mazoea yao binafsi.
Kristo mfufuka anasema Baba Mtakatifu,
anawatuma Mitume wake kutolea ushuhuda wa uwepo wake unaoyakomboa mataifa, kwani Mwenyezi
Mungu ni mwingi wa upendo na anataka kila mtu aweze kuokoka na kamwe asipotee! Vijana
wanaalikwa kufungua macho yao ili kuona makando kando yao. Mataifa wanayoalikwa kuyatangazia
Habari Njema si nchi nyingine duniani; bali ni kila sehemu ya maisha yao; kama vile
familia, jumuiya mahali pa masomo na kazi; makundi ya marafiki zao na “vijiwe” wanapotumia
muda wao wa ziada. Utangazaji wa Injili ya Kristo kwa njia ya furaha inamaanisha kugusa
kila sehemu ya maisha.
Baba Mtakatifu anapenda kukazia kwa namna ya pekee,
Uinjilishaji katika sekta ya mawasiliano ya jamii, hasa katika mtandao, unaotumiwa
kwa kiasi kikubwa na vijana, wanaotekwa kwa urahisi zaidi na njia za mawasiliano ya
jamii, ili kuweza kuwajibika katika kuuinjilisha ulimwengu wa mtandao.
Sehemu
ya pili ni safari na uhamiaji, kwani vijana wengi wanasafiri kwa sababu mbali mbali
kama vile masomo na kazi na wakati mwingine ni kwa ajili ya kujifurahisha. Lakini
pia kuna mamillioni ya watu, wengi wao wakiwa ni vijana, wanaosafiri kutoka sehemu
moja hadi nyingine wakitafuta fedha au kutokana na sababu mbali mbali za kijamii.
Hili linaweza kuwa ni jukwaa pia la kushirikishana Injili.
Baba Mtakatifu anawakumbusha
vijana kwamba, kutangaza habari Njema ya Wokovu ni dhamana inayohusu maisha yao yanayogeuzwa
kuwa ni alama za upendo, unaofanana na ule wa Kristo. Vijana wanapaswa kujiandaa vyema
kama yule Msamaria mwema, kwa kuwa makini kwa watu wanaokutana nao, ili kuwasikiliza,
kuwaelewa na kuwasaidia. Kwa njia hii wanaweza kuwaongoza watu wanaotafuta maana ya
maisha kwenda nyumbani mwa Mungu, yaani Kanisa, mahali ambapo matumaini na wokovu
ni makazi yake.
Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Katekesi makini, wanaweza
kuwafanya wengine kuwa ni wafuasi, kwa kuwaongoza wengine ili waweze kukutana na Yesu
Kristo kwa njia ya Neno na Sakramenti zake. Kwa njia hii, wanaweza kumwamini na kupata
fursa ya kuweza kumfahamu Mungu na hatimaye, kuishi katika neema yake. Baba Mtakatifu
anawaalika vijana kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwasaidia; kuwaonesha njia ya
kumfahamu na kumpenda Kristo kwa ukamilifu zaidi, wakijitahidi kuwa wagunduzi wanapotangaza
Injili.
Baba Mtakatifu anawatia moyo vijana kamwe wasikate tamaa wanapojisikia
kwamba ni dhaifu na wanyonge kiasi cha kushindwa kuinjilisha, wasikate tamaa, bali
watambua kwamba, uinjilishaji si utume unaotegemea karama na uwezo wao. Wanapaswa
kuwa waaminifu na watii ili kuitikia wito unaojikita katika nguvu ya Mungu. Vijana
wanatakiwa kuyasimika maisha yao katika sala na maisha ya Kisakramenti, kwani uinjilishaji
wa kweli ni matunda ya sala na unaenziwa pia kwa sala.
Vijana wajifunze kuzungumza
na Mungu ili hatimaye, waweze kuzungumza kuhusu Mungu. Maisha ya imani ya vijana yapate
chimbuko lake katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, pamoja na kujitahidi
kupokea Sakramenti ya Upatanisho mara kwa mara. Kwa wale ambao bado hawajaimarishwa
kwa Sakramenti ya Kipaimara, waongeze juhudi ya kuipokea sakramenti hii, kwani kama
ilivyo pia Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni Sakramenti za utume, kwani zinawakirimia
nguvu na mapendo ya Roho Mtakatifu ili kuweza kuungama imani. Vijana wanaalikwa kushiriki
kikamilifu katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu.
Ikiwa kama vijana watafuata
njia hii kwa ukamilifu, Yesu mwenyewe atawawezesha kuwa waaminifu kwa Neno ili waweze
kutolea ushuhuda amini na wenye nguvu kwake Yeye. Wakati mwingine watajaribiwa ili
kuonesha udumifu, pale neno la Mungu linapokatiliwa au kukumbana na upinzani. Baba
Mtakatifu anatambua mateso na dhuluma ambayo baadhi ya vijana wanakabiliana nazo sehemu
mbali mbali za dunia kiasi kwamba, hawawezi hata kidogo kutolea ushuhuda wa imani
yao kwa Kristo na Kanisa lake kutokana na ukosefu wa uhuru wa kidini. Kuna baadhi
yao ambao tayari wamekwisha yamimina maisha yao kwa sababu tu ni Wakristo. Baba Mtakatifu
anawataka vijana kuwa imara katika imani yao, daima wakitambua kwamba, Yesu Kristo
yuko pamoja nao katika kila jaribu la maisha.
Vijana wanalihitaji Kanisa ili
kuweza kuwa imara katika imani yao ya Kikristo. Hakuna mtu anayeweza kutolea ushuhuda
wa Injili peke yake, kwani Yesu aliwatuma wafuasi wake kwa pamoja. Hivyo, ushuhuda
wa imani daima unatolewa ba Jumuiya ya Kikristo na utume wao unaweza kuzaa matunda
kwa njia ya umoja unaomwilishwa ndani ya Kanisa. Ni kwa njia ya umoja na upendo kwa
jirani, wengine wanaweza kuwatambua kwamba, wao ni wafuasi wa Kristo.
Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya siku ya
vijana duniani kwa mwaka 2013 anawaalika vijana kusikiliza kutoka katika undani wa
mioyo yao sauti ya Yesu inayowaita kutangaza Injili. Kama sanamu ya Yesu Kristo Mfalme
inavyoonesha pale Rio de Janeiro, ni moyo ambao umefunguka kwa upendo kwa kila mtu
na mikono yake iko wazi kuwafikia watu wote. Ni changamoto kwa vijana wenyewe kuwa
ni moyo na mikono ya Yesu, kwa kutolea ushuhuda wa upendo huu sanjari na kuwa ni wamissionari
kwa vijana wa kizazi kipya, wanaowajibishwa na upendo ambao uko wazi kwa wote.
Baba
Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa kusema kwamba, mwaliko anaoutoka kwa vijana
ni kwa ajili ya dunia nzima, lakini zaidi kwa vijana wanaoishi Amerika ya Kusini.
Katika maadhimisho ya mkutano wa tano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Amerika
ya Kusini, uliofanyika mjini Aparecida kunako mwaka 2007, Maaskofu walizindua kampeni
ya utume Barani humo. Vijana wanaunda idadi kubwa ya wananchi wa Amerika ya Kusini.
Hawa ni rasilimali muhimu sana kwa Kanisa na Jamii, changamoto ya kutangaza kwa ari
zaidi imani kwa vijana wenzao kutoka sehemu mbali mbali za dunia.