2012-12-13 10:08:00

Kifo cha Rais Samora Machel wa Msumbiji kunako mwaka 1986 kuchunguzwa tena!


Serikali ya Afrika ya Kusini imeanza kufanya uchunguzi upya kuhusiana na ajali ya ndege iliyosababisha Rais Samora Machel wa Msumbiji kupoteza maisha kunako mwaka 1986. Hii inatokana na ukweli kwamba, Rais Machel alikuwa ni kati ya viongozi waliokuwa Kusini mwa Afrika waliosimama kidete kupinga na kulaani wazi wazi utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini kwa wakati huo. Uchunguzi wa kwanza uliofanywa na Serikali ya Afrika ya Kusini kwa kushirikiana na Serikali ya Msumbiji haukubainisha ukweli wote.

Hayo yamethibitishwa na Paul Ramaloko, Msemaji mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Afrika ya Kusini, aliyethibitisha kwamba, Afrika ya Kusini na Msumbiji vinashirikiana kwa karibu zaidi ili kufanya uchunguzi wa kina utakaobainisha sababu ya ajali ya ndege iliyopelekea Rais Samora Machel wa Msumbiji kupoteza maisha yake. Alikuwa ni kiongozi maarufu na muasisi wa Taifa la Msumbiji aliyeongoza wananchi wa Msumbiji kupigania uhuru wao hadi kufanikiwa kunako mwaka 1975.

Rais Samora Machel pamoja na viongozi wengine 33 walipoteza maisha yao kwa ajali iliyotokea Oktoba 1986, wakati Ndege ya Rais ilipogonga milima wakati inarejea kutoka Zambia. Uchunguzi mpya unaanza kutekelezwa kutoana na madai ya kupatikana kwa ushahidi mpya unaoonesha kwamba, Serikali ya Ubaguzi wa Rangi Afrika ya Kusini, ilihusika kwa namna moja au nyingine.

Serikali ya Afrika ya Kusini wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe iliunga mkono majeshi ya Renamo dhidi ya Serikali ya Frelimo iliyokuwa chini ya Rais Samora Machel. Hii ni vita ambayo iliacha kurasa chungu kwa wananchi wa Msumbiji hadi leo hii.

Itakumbukwa kwamba, kunako Mwaka 1987 Mahakama kuu ya Afrika ya Kusini, iliamua kwamba, ajali ya ndege iliyopelekea kifo cha Rais Samora Machel ilitokana na uzembe wa rubani wa ndege hiyo. Mzee Nelson Mandela mara baada ya kubwagwa kwa utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini kunako mwaka 1994 na kuundwa kwa Tume ya Ukweli na Upatanisho walianza uchunguzi ambao hakufikia hatima yake. Wapenda haki na amani wanasubiri kwa hamu matokeo ya uchunguzi mpya kuhusu ajali ya ndege iliyopelekea kifo cha Rais Samora Machel wa Msumbiji.







All the contents on this site are copyrighted ©.